Kila mtu alipokuwa mdogo alikuwa na picha kubwa sana ya maisha yake.
Ulipokuwa mdogo mtu akikuuliza unataka kuwa nani ulikuwa unajibu bila ya wasi wasi wowote kile unachotaka kuwa.
Ulikuw ana picha kubwa ya maisha yako, vile unataka yawe na kile unachotaka kutoa.
Safari ikaendelea na mahala fulani mambo yakabadilika.
Ukaanza kuambiwa hiki hakiwezekani, huwezi hiki, huna hiki, acha kuota na kadhalika.
Maneno haya uliyapuuza mwanzoni, ila yaliendelea kila siku, ukajaribu kufanya licha ya maneno haya, ukashindwa.
Na hapa ndio kitu kibaya sana kilichotokea, baada ya kushindwa tu, ukakubaliana nao, kwamba walikuwa sahihi, kwamba wewe huwezi, kwamba wewe huna, kwamba wewe unaota ndoto za mchana.
SOMA; Njia 12 za kurahisisha maisha yako.
Na sasa hatimaye unaishi maisha anayoishi kila mtu, huyafurahii lakini unaenda nayo tu, kwa sababu wanazidi kukuambia kwamba hiki ndio ulichopata, shukuru, huwezi kupata zaidi ya hiko.
Huu wote umekuwa ni uongo mkubwa sana uliojazwa kwenye kichwa chako. Wazazi na jamii zimejitahidi kukujengea uwezo huo, mfumo wa elimu ukamalizia kabisa na sasa unaona ndivyo mambo yalivyo.
Sasa leo jiulize swali moja…
Yako wapi yale maisha?
Tatizo letu binadamu ni kwamba kama hatujapata kile tunachokitaka kweli mioyo yetu haiwezi kutulia. Utafanya kila kitu ili kujiridhisha kwamba maisha ni mazuri lakini bado utakuwa na deni. Utajaribu kujiweka kwenye mazingira ya kuonekana una mafanikio kwenye maisha, lakini unapokaa chini na kutafakari maisha yako, utaona kuna deni fulani lipo ndani yako.
Sasa ni wakati wa wewe kulipa deni hilo.
SOMA; Kama Ulikuwa Hujui Bahati Inavyopatikana Soma Hapa.
Maswali muhimu wewe kujiuliza ni;
Je naridhishwa na kazi au biashara ninayofanya sasa?
Je naridhishwa na aina ya maisha ninayoishi sasa?
Je natoa mchango wa maana kwa kile ninachofanya kwenye jamii yangu na dunia kwa ujumla?
Je ningekuwa na uhakika nina mwezi mmoja tu wa kuishi, ningeutumia mwezi huo kufanya nini?
Maswali hayo yatakufungua ujue deni ambalo bado unadaiwa. Ukiweza kulipa deni hili maisha yako yatakuwa ya furaha hata kama huna utajiri mkubwa.
Huu ni wakati wa wewe kulipa deni. Jibu maswali hayo na chukua hatua.
Uzuri ni kwamba kwenye maisha hakuna kuchelewa. Katika wakati wowote ambao umegundua kwamba njia uliyokuwa unaenda siyo, unaweza kuibadili na ukaboresha maisha yako.
Nakutakia kile la kheri,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
SOMA; Hii Hapa Ni Tsh 604,000/= Utakayokabidhiwa Leo Usiku. Utaitumiaje?