Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Saturday, July 18, 2015

Nakukumbusha Kwamba Tumeshahama hapa.

Habari za leo mpenzi msomaji wa blog hii.
Napenda kukumbusha kwamba blog hii sasa imehama na makala zotye zinapatikana kwenye www.kisimachamaarifa.co.tz
Kwa wale ambao walikuwa wanapokea makala kwa email, unapoenda kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuna sehemu ya kuweka email yako ili uendelee kupata makala kila zinapotoka.
Nakutakia kila la kheri.
TUPO PAMOJA.

Friday, July 17, 2015

UKURASA WA 198; Tuko Upande Mmoja.

Katika shule moja kulikuwa na kundi la wanafunzi watukutu ambao walikuwa wakionea wanafunzi wenzao. Wanafunzi hao walikuwa wakikuta mwanafunzi mwingine wanamlazimisha achague wa kupigana naye na akikataa wanampiga wote.
Siku moja kundi hili walikutana na mwanafunzi mmoja aliyeonekana kuwa mnyonge sana. Wakamwambia achague wa kupigana naye. Yule mwanafunzi akachora mstari na kusema yule ambaye anajiona ndio mbabe kuliko wote avuke huu mstari. Yule ambaye ndio alikuwa mbabe alivuka mstari ule na alipofika upande wa pili yule mwanafunzi mnyonge alimwambia sasa tupo upande mmoja, tuungane kupambana na hao wengine.
Maisha ndivyo yalivyo, sisi wote tuko upande mmoja. Na watu wote wanaokuzunguka mpo nao upande mmoja. Sema watu hatuelewi hili na ndio maana tumekuwa tunashindana lakini hatufiki mbali.
Kama wanandoa wangejua kwamba wapo upande mmoja, wa kutaka maisha yao wote kuwa bora basi matatizo mengi sana ya ndoa yasingekuwepo na ndoa zingedumu.
Kama mwajiri na mwajiriwa wangejua wapo upande mmoja, kunufaisha kazi yao na maisha yao kwa ujumla, basi kungekuwa na ufanisi mkubwa sana kwenye eneo la kazi.
Kama mfanyabiashara na mteja wake wangejua kwamba wapo upande mmoja basi biashara zingeendeshwa kwa mafanikio makubwa kwa wote wawili.
Lakini mara nyingi tunafikiri kwamba tuko pande tofauti na hivyo kuishia kushindana, mashindano ambayo hayamfaidishi hata mmoja wetu.
TAMKO LA LEO;
Najua kwamba wale wote ambao wamenizunguka tupo upande mmoja. Mwenza wangu, wateja wangu, mwajiri/mwajiriwa wangu wote tupo upande mmoja. Kila mara nitajitahidi kuelewa upande tuliopo ili iweze kutusaidia kuboresha maisha yetu sote.
Tukutane kwenye ukurasa wa 199 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Tangazo muhimu kuhusiana na blog zinazoendeshwa na AMKA CONSULTANTS.

Habari za leo mpenzi msomaji wa blog mbalimbali zinazoendeshwa na AMKA CONSULTANTS. Naamini unaendelea vizuri na harakati zako za kuboresha maisha yako. Na pia naamini TUPO PAMOJA ukiendelea kujifunza na kuhamasika kupitia makala mbalimbali zinazopatikana kwenye blog zako zinazoendeshwa na AMKA CONSULTANTS.
Kama unavyojua lengo kubwa la AMKA CONSULTANTS ni kukuwezesha wewe kuishi maisha bora sawa sawa na uwezo wako. Hapo ulipo una uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa zaidi ya unavyofanya sasa. Ila mfumo wa elimu uliopitia na malezi uliyokulia vimekufanya ushindwe kufikia uwezo wako mkubwa.
Kama umekuwa unafuatilia blog zetu mbali mbali na ukawa unafanyia kazi yale ambayo umekuwa unajifunza, utakubaliana nami kwamba maisha yako umeona yanabadilika, hata kama ni kwa kiasi kidogo. Kama hiki ndio kinachotokea kwenye maisha yako basi nakusihi endelea kufanyia kazi na utazidi kuona mabadiliko makubwa zaidi.
AMKA CONSULTANTS ilianza na blog ya AMKA MTANZANIA na baadae zilianzishwa blog nyingine kutokana na mahitaji tofauti ya wasomaji wetu. Blog hizo ni KISIMA CHA MAARIFA, ambayo unalipia kuwa mwanachama, MAKIRITA AMANI na JIONGEZE UFAHAMU.
Kupitia blog hizi umekuwa unajifunza mambo mengi na mazuri sana. Kwa sababu makala zinazowekwa kwenye blog hizi zinatofautiana na zinalenga maeneo tofauti tofauti ya maisha yako ikiwemo kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwajulisha wasomaji wote kwamba kutakuwa na mabadiliko kwenye blog hizi zinazoendeshwa na AMKA CONSULTSNTS. Makala ambazo zilikuwa zinawekwa kwenye JIONGEZE UFAHAMU sasa zitahamishiwa kwenye AMKA MTANZANIA na makala zilizokuwa zinawekwa kwenye MAKIRITA AMANI sasa zitahamishiwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Na blog hizi mbili, MAKIRITA AMANI na JIONGEZE UFAHAMU zitafutwa.
Kwa nini mabadiliko haya?
Kama umekuwa msomaji mzuri wa blog hizi utakuwa uliona tatizo ambalo lilijitokeza kama mwezi mmoja uliopita. Wasomaji ambao walikuwa wanapokea makala za blog moja wapo kwa email ghafla waliacha kupata makala. Wakati huo makala zilikuwa zinatumwa kama kawaida. Kutokana na tatizo hili ilibidi kutafuta suluhisho la haraka ili wasomaji waendelee kupata makala zetu nzuri. Tulipata suluhisho la muda lakini halitadumu kwa muda mrefu, siku zio nyingi tutaingia tena kwenye tatizo kama lile. Na hii inatokana na sababu ya pili ya kuondoka kwenye blog hizi ambayo ni kuwa zimekuwa zinaendeshwa bure.
Blog inapokuwa imehifadhiwa bure na kutumia jina la bure, kuna baadhi ya vitu huwezi kuvibadili. Sasa hili linakwenda tofauti na kile ambacho nataka wewe msomaji ukipate. Kuna wakati nataka kufanya kitu ambacho ni cha tofauti lakini nashindwa kwa sababu blog imehifadhiwa bure na hivyo huwezi kubadili baadhi ya vitu.
Sababu nyingine ni kwamba nina sehemu kubwa ya kuhifadhi blog hizi ambayo ninailipia kila mwaka ambayo kwa sasa imehifadhi KISIMA CHA MAARIFA, sasa ni vyema kutumia sehemu hii ambayo tunailipia gharama kubwa kuweka mafunzo ambayo yataendelea kuboresha maisha yako.
Na sababu ya mwisho tunayoweza kujadili hapa ambayo imepelekea kufanya mabadiliko haya ni wewe msomaji uweze kupata makala zote nzuri kwenye blog chache. Ni kweli kuna umuhimu wa kutenganisha mambo lakini ni vyema wewe kama msomaji ukijua unapata makala zako zote nzuri kwenye sehemu chache ambazo unaweza kuzitembelea kila siku na kutumia muda wao vizuri.
KISIMA CHA MAARIFA ni kulipia, je sisi tuliokuwa tunapata makala bure ndio mwisho?
Ni kweli kabisa ili uweze kusoma makala kwenye KISIMA CHA MAARIFA inabidi uwe umejiunga na ulipie. Ila kwa sasa kwa kipengele hiki cha KURASA 365 ZA MWAKA 2015 wasomaji wote wataendelea kuzipata hata kama hawajajiunga na kulipia. Ila nakusihi sana kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA ufanye hivyo mara moja kwani unakosa mengi na utaendelea kukosa mengi. Bonyeza maandishi haya KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA. Kuendelea kupata makala za KURASA 365 hakikisha unatembelea KISIMA CHA MAARIFA kila siku, na pia jiunge kwa kuweka email yako unapokuw akwneye KISIMA na utatarifiwa kila makala inapokwenda hewani.
Asante sana kwa kuendelea kujifunza na kufanyia kazi yale ambayo yanawekwa kwenye mitandao hii. Tunaendelea kukuahidi kwamba tutakuletea makala bora kabisa zitakazo boresha na kubadili maisha yako.
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Thursday, July 16, 2015

UKURASA WA 197; Una Sababu Moja Tu, Nyingine Zote Ni Kuchagua.

Umekuwa ukisikia mara nyingi kwamba kosa sio kutenda kosa, bali kosa ni kurudia kosa. Hii ikiwa na maana kwamba unapofanya jambo kwa mara ya kwanza na ukapata majibu ambayo hukutegemea kupata, tunaweza kukusamehe. Ila tunatarajia kwamba uwe umejifunza kwamba njia uliyotumia mwanzo haileti majibu unaotaka.
Sasa kama wewe utarudia tena kufanya vile vile na ukapata majibu yale yale ambayo hukuyataka ndio tunasema kwamba wewe unafanya makosa. Nafikiri tumeelewana vizuri hapo kwenye kosa, na unajua ni makosa gani ambayo umechagua kuwa unayafanya tena na tena.
Sasa leo nataka nikuambie kitu kingine kizuri ambacho kinaweza kuendana na hiko. Una sababu moja tu, nyingine zote ni kuchagua mwenyewe. Kwa maana nyingine unaweza kuwa na kisingizio mara moja tu, baada ya hapo umeamua mwenyewe na huna sababu au kisingizio chochote.
Kwa mfano; kwa nini kila siku unasema utaanza biashara ila huanzi? Sababu ya kweli, sina mtaji. Swali hilo tena miaka mitano baadae, kwa nini mpaka sasa hujaanza biashara... hapa ukisema tena huna mtaji sio sababu tena, maana yake unajua kabisa kwamba huna mtaji na hufanyi jitihada zozote kutafuta mtaji huo.
Usipende kutafuta sababu(visingizio), ila kama haikwepeki, basi sababu iwe mara moja tu. Kama utaendelea kutuambia sababu ile kila siku sio sababu tena bali umeamua kuishi maisha hayo. Hivyo tafadhali sana, usitupigie tena kelele, tumeshasikia sababu yako na umeshatuambia kwamba umekubali kuishi nayo.
TAMKO LA LEO;
Najua nina nafasi moja tu ya kuwa na sababu au kisingizio. Ila baada ya hapo siwezi tena kutumia kisingizio hiko kwa sababu nitakuwa nimeamua mwenyewe. Kuanzia leo nitakwepa kutoa sababu na kama sababu haikwepeki nitatoa mara moja tu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Wednesday, July 15, 2015

UKURASA WA 196; Kama Huwezi Kujibu Swali Hili Hujui Maisha Yako Yanakoelekea.

Siku zote huwa nasema kwamba kuna ‘emergency’ chache sana kwenye maisha. Ile hali kwamba jambo limetokea na watu wanashangaa limetokeaje ni kuamua tu kutumia unafiki wetu wenyewe.
Ni sawa na shimo ambalo lipo njiani kwa muda mrefu lakini watu wanaliangalia tu, siku moja linasababisha vifo watu wanasema ni ajali. Hapana sio ajali, ni watu wamechagua kufa kwa njia hiyo. Kwa sababu shimo lilikuwa linaonekana siku zote, lakini hakuna aliyejali.
Hivyo hivyo kwenye maisha yako, kuna vitu vingi sana ambavyo unavipuuzia kwa sasa lakini kuna siku vitakukaba sana. Na wakati huo ndio utaanza kuhangaika, utaanza kusumbua wengine kwamba kwa nini hawachukulii hali yako kwa tahadhari. Bila ya wewe kujua na kukubali kwamba hakuna tahadhari kubwa ila ni kitu ulichotengeneza wewe mwenyewe.
Kila siku inayoanza jiulize swali hili muhimu sana, je mambo haya ninayofanya leo hayatengenezi tahadhari siku ya kesho? Au siku zijazo? Mambo ninayoyapuuza leo hayajitengenezi na kuwa makubwa halafu siku moja yakanizidi?
Ni kawaida ya binadamu kufanya vitu kwa mazoea ila mambo yanapokuwa magumu tunasahau kwamba tumeyatengeneza wenyewe. Na kama wewe ni mtu wa kulaumu utaanza kulaumu na uzuri ni kwamba hutakosa mtu wa kumlaumu.
Hakuna kitu kinachokea kwa ajali kwenye maisha yako, kila kitu kinasababishwa na wewe mwenyewe ndiye unayesababisha. Kuwa makini na yale yote unayofanya, yanaweza kukusababishia matatizo makubwa siku za mbeleni.
TAMKO LA LEO;
Najua chochote ninachofanya leo kina madhara kwenye maisha yangu siku za baadae. Madhara haya yanaweza kuwa chanya au kuwa hasi. Nitahakikisha maamuzi ninayofanya hayanipelekei kwenye madhara hasi ili niepuke kuwa na dharura zisizo za msingi kwenye maisha yangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa 196 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Tuesday, July 14, 2015

UKURASA WA 195; Dunia Inapenda Washindi, Usiumizwe Na Hilo.

Wakati unaweka juhudi za ziada zaidi ya wengine hakuna atakayekutukuza, na wengine wengi watakukatisha tamaa.
Wakati wewe unafanya kazi wakati wengine wamepumzika, wanastareheka hakuna atakayekuwa anakumulika, na wanaojua watakuwa wanakubeza na kukuona hujui unachofanya.
Kama utaendelea kung’ang’ana na kuweka juhudi licha ya watu kukususa na wengine kukukatisha tamaa, unajua ni nini kitatokea?
Mambo yako yatakuwa mazuri, utaanza kupata majibu tofauti na wengine wanayopata, kila mtu ataanza kuona mafanikio yako. Na wakati huu unajua ni kitu gani kitatokea?
Kila mtu ataanza kukutukuza, kukusifu, huyu hakukata tamaa. Na wanaokujua wataanza kusema tulijua tu atafika mbali, wakati hakuna hata siku moja wamekutia moyo.
Je utawachukia watu hawa kwa sababu ni wanafiki, wanakusifia wakati tu umefikia mafanikio? Hapana usifanye hivyo, sio kosa lao, ndivyo dunia ilivyowatengeneza. Dunia inapenda washindi, dunia haina muda na wanaoteseka, wanaokazana na ukishindwa ndio kabisa utakuwa mfano wa kuwatisha wengine.
Ufanye nini sasa? Endelea kuweka juhudi, endelea kushinda. Hata pale wanapokusifia usione ndio umefika mwisho, wacha wao waendelee kutoa sifa, na wewe endelea kuweka juhudi.
TAMKO LA LEO;
Najua dunia inapenda washindi. Hainisumbui kama sasa hivi hakuna anayeniona pamoja na juhudi kubwa ninazoweka. Na hata nitakapofikia mafanikio na waliokuwa wa kwanza kunicheka wakawa ndio wa kwanza kusema walijua nitafanikiwa pia halitakuwa tatizo kwangu. Mimi nitaendelea kuweka juhudi bila ya kujali watu wanasema nini.
Tukutane kwenye ukurasa wa 196 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Monday, July 13, 2015

UKURASA WA 194; Utaanza kuona fursa nzuri pale utakapofanya hivi.

Hivi ulishawahi kununua nguo ambayo uliona ni nzuri na ya kipekee ila kila ulipopita mtaani ukaanza kuona karibu kila mtu anayo?
Au labda unafikiria kununua kitu fulani mfano gari au vifaa, mara ghafla ukiwasha tv unaona kitu kile, ukipita mtaani unaona kitu kile?
Au umewahi kufikiria kufanya biashara fulani mara ghafla ukaanza kuona kila unapopita unaona watu wanafanya biashara ile?
Je unafikiri vitu hivyo nimeanza kutoke kwa sababu wewe unafikiria kufanya? Jibu ni hapana, vitu hivyo vilikuwepo kila siku, ila kwa sababu hujawahi kuvifikiria na kuvizingatia basi umekuwa huvioni. Ila unapoanza kuvifikiria au kuvizingatia sana macho yako yanafunguka na unaanza kuona vizuri zaidi.
SOMA; Huwezi Au Hutaki? Kabla Hujaniambia Huwezi, Hakikisha Huponi.
Kuna fursa nyingi sana ambazo zinakuzunguka hapo ulipo. Ila kwa sasa huzioni kwa sababu hujazingatia kuzifikiria. Anza kufikiria kitu fulani na utaanza kuona kwamba kuna njia nyingi sana za kuweza kukipata au kukifanya kitu hiko?
Unataka kuona fursa zaidi? Fungua akili yako, fungua mawazo yako na macho yako yataanza kuona.
TAMKO LA LEO;
Najua nimekuwa sioni fursa nyingi kwa sababu macho yangu hayajafunguliwa kuona. Nitayafungua sasa macho yangu kwa kuzingatia vitu ninavyotaka, kuviweka kwenye akili yangu na macho yangu yatanionesha njia za kufanya au kupata vitu hivyo.
Tukutane kwenye ukurasa wa 195 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Sunday, July 12, 2015

UKURASA WA 193; Ushabiki Unavyokuzuia Kufikia Mafanikio.

Ushabiki umekuwa kikwazo kwa watu wengi sana kuweza kufikia mafanikio makubwa. Watu wamekuwa wakijikuta wanalazimika kuacha mambo yao ya msingi kwa sababu hataki kupitwa na kitu ambacho anashabikia.
Kuna watu ambao ni mashabiki wa mpira kiasi kamba hawezi kuacha kuangalia timu yake inacheza hata kama kutakuwa na kitu gani anachofanya. Kuna wengine ni mashabiki wa muziki, mashabiki wa tamthilia, mashabiki wa matamasha mbalimbali na pia mashabiki wa siasa.
Sina tatizo na wewe kuwa shabiki, ila kama kweli lengo lako ni kuwa na maisha bora na yenye mafanikio basi unatakiwa kufikiria mara mbili kuhusu ushabiki wako.
Fikiria kile unachoshabikia na jiulize, je kinakuongezea maarifa? Je kinakuongezea kipato? Je kinafanya maisha yako na ya wengine kuwa bora zaidi/ kama jibu ni hapana basi ushabiki huo usiwe kipaumbele kwenye maisha yako.
SOMA; Huwezi Au Hutaki? Kabla Hujaniambia Huwezi, Hakikisha Huponi.
Mimi nilikuwa mshabiki wa tamthilia mpaka siku moja mtu akaniambia(kupitia kitabu nilichokuwa nasoma), unapoangalia tv, kuna mambo mawili yanatokea. Yule unayemwona kwenye kioo cha tv analipwa kwa wewe kumwangalia na wewe unalipa kumwangalia mtu huyo. Je unataka kuwa upande upi? Kulipa uangalie maisha ya wengine au kulipwa kwa watu kuangalia maisha yako? Kuanzia hapa nilikata shauri la kutoangalia tamthilia tena, sijaziangalia tangu mwaka 2012 na hakuna nilichokosa zaidi ya maisha yangu kuwa bora zaidi.
Achana na ushabiki ambao hautaboresha maisha yako na anza leo kuwa shabiki wako mwenyewe. Mimi ni shabiki namba moja wa Makirita Amani, huwa sikosi chochote alichopanga kufanya na nitaahirisha vingine vyote ili kuhakikisha namshabikia. Je shabiki wako namba moja ni nani?
Una muda mfupi sana kuanza kuugawa kwa kushabikia vitu ambavyo havina msaada mkubwa kwenye maisha yako, hasa ambavyo unaweza kuvipata baadae. Kwa mfano kama unashabikia timu ya mpira, badala ya kukesha ukiangalia mpira na kesho yake ukashindwa kufanya kazi zako vizuri kwa nini usilale mapema na kesho yake utayajua tu matokeo? Hakuna tofauti yoyote kuona magoli mawili yakifungwa na kuja kuyaona kesho yake. Tena siku hizi mipira inarekodiwa kwa hiyo unaweza kuangalia kwa muda wako.
Narudia tena, usikubali ushabiki uharibu ratiba zako, una mengi yakufanya, yape kipaumbele.
TAMKO LA LEO;
Najua ushabiki wangu umekuwa unanifanya nishindwe kufikia mafanikio makubwa. Nimekuwa nashabikia mambo mengi sana. Nimekuwa naahirisha mipango yangu kwa sababu tu nisipitwe na ushabiki. Leo naamua kwamba mtu wa kwanza kumshabikia ni mimi mwenyewe. Sitakatisha ratiba zangu kwa sababu kuna kitu nakishabikia. Nitaendelea na mipango yangu na ninajua nitafahamishwa kila kinachoendelea.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Saturday, July 11, 2015

UKURASA WA 192; Tatizo La Kuweka Kipimo Cha Furaha, Na Kwa Nini Hukifikii.

Kuna watu ambao huwa wanaweka furaha kwenye kipimo. Mtu anafikiri nikishapa kitu fulani basi nitakuwa na furaha sana.
Kwa hiyo huwa inaanza hivi;
Uko mtoto mdogo unatamani sana kwenda shule unasema nikianza darasa la kwanza nitafurahi sana. Unaanza na unagundua hakuna kitu cha tofauti sana.
Unaendelea na shule kwa miaka saba, unapokaribia mwisho unasubiri kwa hamu sana ukisema nikimaliza darasa la saba tu, nitakuwa na raha sana. Unamaliza na unaona kumbe kilikuwa kitu cha kawaida sana.
Unaanza sekondari unasoma na kufikiria nikimaliza tu, nitakuwa na raha, unamaliza na maisha ni yale yale.
SOMA; Ndege Wa Angani Hawalimi Ila Wanakula, Kuna Mambo Haya Matano(5) Pia Wanakuzidi Ujanja.
Hivyo hivyo mpaka unaingia chuoni, unafikiria nikimaliza na nikapata kazi, maisha yangu yatakuwa ya furaha sana. Unamaliza na labda unapata kazi na unakuta ni kawaida tu na huenda ukakutana na changamoto nyingi zaidi.
Hivyo pia inakuwa kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, unafikiri ukipata kitu fulani utakuwa na furaha, ila unakifanya na unagundua kuna kingine zaidi cha kufanya.
Ni vigumu sana kupima furaha kwa vipimo hivi hasa pale unaposogeza kipimo kila unapokifikia.
Wakati sahihi kwako kuwa na furaha ni sasa hivi, hapo ulipo na unaposoma hii. Na utakapotoka hapo kila wakati kuwa na furaha. Kama unafikiria utaipataje furaha chukua kalamu na karatasi na andika vitu kumi unavyoshukuru kuwa navyo hapo ulipo. Huenda ni kazi au biashara inayokupatia fedha za kuendesha maisha, huenda ni familia inayokupenda, huenda ni marafiki mnaopendana na kadhalika.
Huwezi kupima furaha na ukaipata, furaha ipo ndani yako, ni wewe kuifikia na kuiishi.
TAMKO LA LEO;
Kuanzia sasa naacha kupima furaha kwa sababu nimegundua kwamba kuweka kipimo kwenye furaha ni sababu namba moja ya kushindwa kuifurahia. Hapa nilipo nina furaha kwa sababu nina vitu hivi vifuatavyo(soma orodha yako ya vitu kumi).
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Friday, July 10, 2015

UKURASA WA 191; unalipwa kwa sababu unaonekana au kwa sababu unatoa thamani?

Swali muhimu sana hilo kujiuliza kama hujawahi kufanya hivyo. Ngoja nikuulize tena vizuri ili twende sawa,
Je unalipwa mshahara kwa sababu unaonekana kazi au kwa sababu una thamani unayotoa kwenye kazi yako?
Je mteja wa biashara yako ananunua kutoka kwako kwa sababu amekuona na wewe unafanya biashara au kwa sababu kuna thamani anaifuata?
Jipe muda wa kujibu swali hili, maana ndio msingi wako wote wa mafanikio umelala hapo.
Kulipwa kwa kuonekana.
Hapa ni pale unapotegemea malipo kwa sababu tu umeonekana kazini, au kwa sababu tu na wewe unauza. Hivyo kinachotokea ni wewe kujionesha kwamba na wewe upo. Kama ni kazini basi unahakikisha unaonekana una kazi nyingi na upo bize kumbe hakuna thamani kubwa unayotengeneza. Ukiwa mtu wa aina hii inakubidi uonekane una juhudi sana kumbe ukweli sio hivyo.
Kama ni biashara unakazana kutangaza ili uonekane na wewe upo.
Tatizo la kutegemea kipato kwa njia hii ni kwamba huwezi kupata kipato kizuri na huwezi kujiamini.
SOMA; Ukiendelea Na Maisha Haya Watu Watakunyanyasa Sana…
Kulipwa kwa kuongeza thamani.
Hiki ndio wanachofanya watu wote wenye mafanikio. Hawaendi kazini ili waonekane na wao wamekuja, ila wanakwenda pale kuleta mabadiliko. Kuongeza thamani kwenye kile wanachofanya na hivyo kuwanufaisha wengi zaidi.
Kama ni wafanyabiashara wanakazana kutatua matatizo yanayowasumbua wengi. Na kwa kuwa suluhisho lao ni bora watu wanakuwa wanawatafuta wenyewe.
Na kwa upande wa kipato, watu hawa wao wenyewe ndio wanaamua walipwe kiasi gani, wakitaka kuongezwa kipato wanaongeza thamani wanayotoa.
Je umeshajua uko wapi? Kazana kuongeza thamani na sio kukazana kuonekana. Unapokazana kuonekana maana yake unapiga kelele. Unapokazana kuongeza thamani umuhimu wako pia unaongezeka. Na kila mtu atataka kufanya kazi na wewe. Na utaanza kupanga ulipwe kiasi gani.
TAMKO LA LEO;
Najua njia bora ya kutengeneza kipato sio kwa kuonekana bali kwa kuongeza thamani. Kuanzia sasa nitakuwa nakazana kuongeza thamani na sio kuwapigia watu kelele ili wajue kama nipo. Najua nitakapotoa thamani kubwa na kipato changu pia kitaongezeka.
Tukutane kwenye ukurasa wa 192 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.