Jana tarehe 02/10/2015 kulikuwa na tafrani kubwa sana katika maeneo mengi ya jiji la dar es salaam. Tafrani hii ilisababishwa na kikundi cha vijana wanaojiita panya road ambao ni genge la uhalifu linalovamia watu na kupora mali kwa kutumia silaha mbalimbali ambazo sio za moto.
Hofu ya uvamizi wa vijana hao kwa jana ilisambaa kwa kasi sana kwenye maeneo mengi ya dar. Uvamizi ulifanyika maeneo machache ila athari za hofu zilisambaa kwenye maeneo mengi na kuleta matatizo mengi.
Katika eneo ninalokaa, tabata, hofu hii ilifika kwa kasi sana na watu walianza kukimbia hovyo, maduka na bar zilifungwa na bara bara zilibaki nyeupe. Waendesha pikipiki maarufu kama boda boda walikuwa mshari wa mbele kusambaza hofu hii. Kwani walikuwa wanapita mitaani wakikimbiza piki piki na kuwaambia panya road wako karibu na wanakuja.
Kwa kweli lilikuwa ni tukio la ajabu sana hasa ukiangalia wingi, nguvu na hata silaha wanazotumia vijana hawa na jinsi hofu hii ilivyowaathiri wengi.
Najua kila mmoja sasa hivi analaani kitendo hiki, kila mmoja analaumu jeshi la polisi kwa uzembe na kila mmoja anajiuliza serikali inashindwaje kudhibiti kikundo cha vijana wanaotumia mapanga, visu, nyembe na mawe.
Wakati hayo yakiwa ya msingi kufikiria, mimi nimejifunza mambo machache kutokana na tukio hili na mambo haya nashawishika kwamba yatatufanya tuendelee kuwa masikini kwa miaka mingi ijayo.
Jambo la kwanza; Watu ni waoga sana na hofu ni mbaya mno.
Wakati tunapata taarifa hizi watu walikuwa wanakimbia hovyo, maduka na bar vinafungwa na kila mtu alikuwa na heka heka. Muda kidogo tukapata taarifa maeneo mengine kama matano hali ni hiyo hiyo. Sasa nikafikiria hawa vijana wako wangapi kiasi kwamba waweze kuteka magomeni mpaka ubungo mpaka mabibo mpaka tabata kwa wakati mmoja. Kikubwa kilichokuwa kinaendelea ni hofu.
Nilishuhudia mama mmoja anaacha gari na kukimbia kwa miguu, hapo hakuna aliyeona sura ya hao panya road bali ni taarifa tu za uwepo wao.
Hofu hii tuliyoishuhudia kwenye sakata hili la panya road ndio inatufanya tuendelee kuwa masikini. Ni hofu hii inawafanya wengi kuendelea kufanya kazi ambazo hawazipendi na haziwapatii kipato cha kutosha ila kwa hofu kwamba nikiacha kazi hii nitafanya nini wanajikuta wanakubali kuwa watumwa.
Ni hofu hii ambayo inawafanya watu kuogopa kujarimu mambo mapya, kuogopa kuzijaribu fursa mpya zilizopo mbele yao na kung’ang’ania kufanya kile walichozoea kila siku ambacho hakiwazalishii kiasi cha kutosha.
Ni hofu hii hii ambayo inatufanya tuogope kudai haki zetu hata pale zinapovunjwa wazi wazi. Tukiamini kwamba iko siku mambo yatakuwa mazuri na hatimaye maisha yetu kuwa hovyo kila siku zinavyokwenda.
Jambo la pili; Watu ni wabinafsi sana.
Katika sakata hili nilishuhudia kitu kimoja ambacho kiliniumiza sana. Kuna wamama ambao walijifungia saluni na wakati huo akaja mtoto mwenye umri kama wa miaka sita amembeba mdogo wake mgongozi. Mtoto yule akawa anawaomba wamama wale wamfungulie aingie lakini hawakudhubutu kufanya hivyo. Mtoto alibaki nje akilia kwa hofu kubwa iliyokuwa imetanda.
Kama watu wote waliokuwa wanakimbia hovyo wangeacha kujiangalia wao binafsi na wakakaa pamoja sidhani kama kikundi hiki kingeweza kuleta tafrani kubwa kiasi hiki. Kitendo cha kila mtu kujijali yeye zaidi kilitoa nafasi kubwa ya hofu kuendelea kusambaa kwa wengine.
Ubinafsi huu kama taifa unatufanya tuendelee kuwa masikini kwa kipindi kirefu kijacho. Ni ubinafsi huu unasababisha watu wachache kuwa mafisadi wakubwa. Ni ubinafsi huu unaotumika kuwagawa wanaopigania haki na hatimaye kushindwa.
Tunahitaji kupambana na matatizo haya makubwa mawili, hii inahitaji kuanzia kwa kila mwananchi mpaka kwa viongozi.
0 comments:
Post a Comment