Katika ukurasa huu wa kwanza kabisa wa kitabu kipya ambacho ni mwaka 2015 ni muhimu sana kuyakubali maisha yako ili uweze kuyabadili.
Kubali kwamba maisha unayoishi ni ya kwako na wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako.
Wewe ndio dereva wa gari unaloendesha ambalo ni maisha yako.
Wewe kama dereva unaweza kufika safari yako vizuri au unaweza kuishia njiani. Leo ndio siku ya kuamua kwamba unataka kufika safari yako ukiwa salama na huku ukifurahia wakati wa safari.
Fanya uchaguzi muhimu leo wa kujichagua wewe kama kiongozi mkuu wa maisha yako.
Jua kwamba hakuna atakayeweza kukutoa hapo ulipo ila wewe mwenyewe. Yaani kama maisha yako ni nyumba inayoungua basi nina taarifa mbaya kwako; hakuna anayekuja kuuzima moto huo, umeachwa mwenyewe.
Sio ndugu, sio serikali, sio bahati inayoweza kukutoa hapo ulipo. Ni wewe mwenyewe unayeweza kuamua kwamba imetosha sasa na uanze safari ya mabadiliko.
Usijaribu kuiga maisha ya wengine, utaishi maisha magumu sana.
Usijaribu kuyalinganisha maisha yako na ya wengine, utajiumiza sana.
Fanya maamuzi haya muhimu leo na yaishi kila siku kuanzia siku ya leo.
Na hivi ndivyo unavyoukamilisha ukurasa wa kwanza, kwa kukubali kwamba maisha unayoishi ni ya kwako na wewe ndio kiongozi mkuu.
Tukutane kwenye ukurasa wa pili kesho.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini.
0 comments:
Post a Comment