Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Thursday, January 1, 2015

Salamu Za Mwaka Mpya Kutoka Kwa Rais Wa Tanzania Mwaka 2040.

Napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuwatakia watanzania wenzangu wote kheri na hongera ya kuuona mwaka 2015. Sio watu wote walioanza mwaka 2014 wamepata nafasi ya kuuona mwaka 2015, hivyo ni jambo la kushukuru kwa nafasi hii ya kipekee.

Mwaka 2014 huenda ulikuwa mwaka uliokuwezesha kufanikisha mengi na pia kushindwa mengi. Kikubwa cha kuchukua 2014 na kukileta mwaka 2015 na yale uliyojifunza. Katika kila jambo ulilofanikiwa kuna vitu umejifunza na katika kila jambo uliloshindwa kuna vitu vingi umejifunza. Tumia yote uliyojifunza ili mwaka 2015 uwe bora zaidi kwako.

Kama mwaka 2014 kuna vitu ulipanga kufanikisha ukashindwa, hii ina maana kwamba kuna vitu unafanya kwa makosa au kuna vitu hufanyi kabisa. Hivyo kuendelea hivyo hivyo kwa mwaka 2015 utapata majibu yale yale uliyopata mwaka 2014. Kumbuka ujinga ni kufanya jambo lile lile kwa njia ile ile na kutegemea majibu tofauti. Haiwezekani na utazidi kupoteza muda wako.

Mwaka huu 2015 ni mwaka ambao utakuwa na matukio mengi na makubwa kitaifa. Matukio haya mengi yatakuwa chachu muhimu katika maendeleo ya nchi yetu. Mambo mawili makubwa kabisa yatakuwa;

1. Kupigia kura katiba pendekezwa. Sote tunajua katiba ilivyo muhimu kwenye taifa lolote, hivyo tukio la kupigia kura katiba iliyopendekezwa ni tukio muhimu sana.

2. Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Mwaka huu tutapata nafasi ya kuchagua viongozi watakaofanya maamuzi kwa niaba yetu kwa miaka mitano ijayo. Hivyo ni jambo linalohitaji umakini wetu ili tusijekupata viongozi ambao watafanya taifa likose uelekeo.

Matukio haya mawili na mengine yatakayotokea mwaka huu 2015 yameshika hisia za wananchi wengi. Wananchi wengi tunaamini mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yetu yatatokea baada ya kupata katiba mpya na kufanya uchaguzi mkuu. Natoa tahadhari kwamba tusitegemee sana hili, mabadiliko ya kweli yanaanzia ndani yako wewe mwananchi. Kila mwananchi anatakiwa kubadilika ndio taifa liweze kubadilika. Kila mwananchi anatakiwa kupata maendeleo ndio taifa lipate maendeleo. Na kwa bahati mbaya sana sehemu kubwa ya mabadiliko ya nchi haitokani na kile serikali inachofanya, bali kile ambacho kila mwananchi anafanya.

Kitu kingine kikubwa ninachopenda kukigusia kwenye salamu hizi za mwaka mpya ni matatizo mawili makubwa yanayoturudisha nyuma kama taifa. Matatizo haya yamekuwa ndio chanzo cha uzembe na ufisadi mkubwa unaoendelea kwenye nchi hii kwa sasa. Matatizo hayo ni;

1. Kutokufanya kazi kwa bidii na maarifa. Najua watanzania tunachukia sana pale tunapoambiwa sisi ni wavivu, ila hata tukichukia huo ndio ukweli wenyewe. Sehemu kubwa ya wananchi ni wavivu au hawafanya kazi kwa viwango ambavyo wanategemewa kufanya. Kila mtu anatafuta njia rahisi ya kupata fedha. Kila mtu anataka apate kitu pasi na kutoa kitu. Hatimaye hii imetuletea wizi na ufisadi mkubwa kwenye taifa. Najua nikisema ufisadi utakimbilia kwenye ESCROW na EPA, lakini je vipi kuhusu daktari anayetaka rushwa ili amhudumie mgonjwa?

Vipi kuhusu afisa wa kodi TRA anayetaka rushwa ili kumsaidia mtu asilipe kodi stahiki?

Vipi kuhusu mwenyekiti wa serikali ya mtaa anayetaka shilingi elfu mbili ndio akupe barua ya utambulisho?

Vipi kuhusu muuza maziwa anayeweka maji kwenye maziwa ili apate zaidi?

Vipi kuhusu kondakta anayepandisha nauli kwa sababu tu kuna watu wengi wanaotaka kusafiri na usafiri ni wa shida?

Vipi kuhusu mwalimu aliyepangiwa kituo cha kazi ila haonekani kazini?

Vipi kuhusu askari wa usalama barabarani anayetaka rushwa kuruhusu gari ambalo halina sifa za kuwepo barabarani kuendelea na safari? Na baadae lisababishe ajali?

Tukiangalia matukio yote haya tunaona ni jinsi gani sehemu kubwa ya taifa tumemezwa na vitendo vya wizi na ufisadi. Tunapiga kelele kukemea ufisadi mkubwa lakini sisi sisi ndio wa kwanza kufurahia kutoa rushwa ili tupate huduma tunazozitaka kwa haraka.

2. Tatizo la pili ni uadilifu, hili ndio linatumaliza kama taifa na ndio linazaa tatizo na kwanza la kutokufanya kazi kwa bidii na maarifa na hatimaye kujiingiza kwenye wizi na ufisadi.

Ni lazima sisi kama wananchi tuanze kujimulika wenyewe, tuone je matendo tunayofanya kila siku kama yangefanywa kuwa ndio sheria ya nchi nzima nchi yetu ingefika wapi?

Tunakuwa wepesi kuwalaumu viongozi kwa tabia zao mbaya lakini tunasahau viongozi hawa wametoka katikati yetu sisi na hivyo wanapeleka tabia walizokuwa nazo kwenye ngazi za juu zaidi.

Kwa hayo machache nikutakia mwaka mzuri na wenye mafanikio makubwa. Nakusihi sana mwaka huu simamia nguzo hizi tatu muhimu

1. Kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

2. Kuwa mwaminifu, tekeleza kile unachoahidi.

3. Kuwa muadilifu, usimfanyie mwingine kile usichopenda kufanyiwa.

Mwaka huu 2015 AMKA CONSULTANTS imejipanga vizuri ili kufanya kazi na wewe na uweze kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa.

Kila siku tembelea AMKA MTANZANIA ili kujifunza na kuhamasika na uweze kuboresha maisha yako.

Tembelea na ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo utakutana na jumuiya ya watu ambao wamechoka kuwa wa kawaida na wanataka kufanya na kuwa zaidi ya walivyo sasa.

Pia tembelea blog hii MAKIRITA AMANI ambapo utakuwa unapata chakula cha ubongo, mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi na kukuhamasisha kuchukua hatua kwenye maisha yako.

Pata picha hii, leo umekabidhiwa kitabu kitupu kabisa chenye kurasa 365 na unaamua uandike nini kwenye kila ukurasa, je ukurasa wa leo umeandika nini? Na wa kesho je?

Mwaka 2015 ukawe mwaka wa mafanikio makubwa kwako.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

Rais wa Tanzania mwaka 2040.

Tafadhali Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri!
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →
Powered By: BloggerYard.Com

0 comments:

Post a Comment