Katika pita pita zangu kwenye mtandao nimekutana na habari moja ambayo Mh January Makamba alishirikisha watu.
Alikutana na watoto wa mtaani, mmoja anasoma mwingine hasomi. Alimuuliza yule asiyesoma akiwa mkubwa anataka kuwa nani, yeye akajibu anataka kuwa muosha magari.
Habari nzima ni ya kusikitisha, kwa sababu watoto hawa wana maisha magumu sana kama ilivyo kwa watoto wengine wa mtaani.
Lakini kilichonifanya niandike hapa ni jibu la mtoto huyo ambalo limenifanya nifikiri zaidi, na nione kuna shida kubwa kwenye jamii yetu kwa sasa.
Zamani mtoto alikuwa akiulizwa anataka kuwa nani, haijalishi kama ameenda shule au la alijibu bila ya wasi wasi kwamba angependa kuwa rubani, daktari, mwalimu, askari, dereva na mengine mengi.
Kwa sasa naona mashujaa wa watoto wanapungua sana, ndio maana unaweza kuona mtoto mdogo anafikiria akiwa mkubwa awe muosha magari. Hii inaweza kutokana na ukweli kwamba watu pekee anaowaona karibu yake ni waosha magari, au jamii imeshamwambia kwamba watu wa aina yako wanaishia kuosha magari.
Hatudharau kazi ya kuosha magari, maana kuna wanaoifanya kitaalamu na inakuwa biashara nzuri. Ila kwa akili ya mtoto na kwa mazingira ya kitanzania wote tunajua kwamba uosha magari anaoufikiria yeye ni upi.
Lengo la makala hii na wito wangu ni turudi kujenga mashujaa kwa vizazi vijavyo. Fanya kazi unayofanya au biashara unayofanya kwa ubora wa hali ya juu kiasi kwamba mtoto wako au wa jirani yako au wa ndugu yako atatamani sana kuwa kama wewe.
Ila kama wewe baba au mama au ndugu kazi yako ni chanzo kikuu cha matatizo kwako hakuna mtoto atakayependa kuishia kwenye matatizo kama yako.
Je upo tayari kuwa shujaa wa mtoto mmoja tu? Tuanze na tutaona mabadiliko makubwa kwenye jamii zetu.
0 comments:
Post a Comment