Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Sunday, May 31, 2015

UKURASA WA 151; Je Unazalisha Au Wewe Ni Mtumiaji Tu?Katika dunia tunayoishi, kuna makundi mawili ya watu. Kuna kundi la watu ambao ni wazalishaji, hawa ni watu ambao wanatuletea vitu vyote tunavyotumia. Simu, tv, vyakula vizuri, vitabu, makala tunazosoma, nguo tunazovaa, magari na vingine vingi. Kundi la pili ni la watumiaji. Hawa ni watu ambao wanatumia vitu hivi vinavyotolewa na wazalishaji.
Kwanza kabisa kila mmoja wetu ni mtumiaji wa kitu kinachotengenezwa na wengine. Huu sio ulimwengu ambao unaweza kujitegemea wewe mwenyewe kwa kila kitu. Unategemea vitu vingi sana kutoka kwa wengine ili maisha yako yaweze kwenda vizuri.
Swali kubwa la kujiuliza ni je wewe unazalisha nini? Ndio umekuwa mtumiaji mzuri, lakini ni kitu gani ambacho unazalisha kwa ajili ya wengine? Unatumia simu nzuri na kuifurahia ila kumbuka kuna mtu amekaa chini, usiku na mchana kutengeneza simu hiyo nzuri unayoipenda leo. Je wewe ni kitu gani kimekuchukua usiku na mchana kufanya na kikafika kwenye mikono ya watumiaji wakafurahi sana? Unavaa nguo nzuri na kujiona unakwenda na wakati, umependeza, lakini kuna watu ambao wamefanya kazi kubwa sana mpaka wakaweza kuja na nguo hizo.
Kazi yako au biashara yako ilikuwa iwe sehemu nzuri sana ya wewe kuzalisha, lakini je unazalisha kupitia hiko unachofanya? Ni kweli unahangaika usiku na mchana kuhakikisha kile unachozalisha kikimfikia mtu atakifurahia sana? Je unatoa kile kilicho bora sana na kujisukuma zaidi ili kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi? Kama ambavyo wengine wanafanya kwenye maisha yako?
Wakati mwingine unapoangalia kitu kizuri unachotumia, jiulize ni kitu gani wewe umezalisha na mtu anayekitumia anafurahia kama wewe unavyofurahia kilichozalishwa na wengine. Hii ikupe hasira ya wewe kuzalisha kilicho bora zaidi. Usikubali kuwa mtumiaji tu, kuwa mzalishaji pia.

TAMKO LA LEO;
Nimechoka kuwa mtumiaji na kufurahia vitu vilivyozalishwa na wengine tu. Sasa na mimi nitakuwa mzalishaji ambaye natoa vitu wengine watavifurahia na kuboresha maisha yao. Nitafanya hivi kupitia kazi au biashara ninayofanya. Najua sijayaishi maisha yangu kama sijaweza kuyabadili maisha ya mwingine kupitia ninachofanya.

Tukutane kwenye ukurasa wa 152 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Saturday, May 30, 2015

UKURASA WA 150; Sababu Moja Inayokufanya Unakwama.Moja ya vitu vizuri nilivyojifunza kwenye maisha ni kwamba, watu huwa wanayafanya maisha yao kuwa magumu wao wenyewe. Yaani kama unaona maisha yako ni magumu, basi wewe mwenyewe umechangia sehemu kubwa sana ya ugumu huo. Unaweza kukataa na kusingizia kila kitu unachoweza, serikali ambayo haitoi ajira, uchumi ambao ni mgumu, wazazi ambao hawakukujali, ndugu ambao hawataki kukusaidia na mengine mengi unayoweza kufikiria.
Kuna sababu moja kubwa sana inayokufanya unaendelea kukwama kila siku kwenye maisha yako na hii inafanya maisha yawe magumu kwako. Sababu hii ni kwamba unajaribu kuwa mtu ambaye siye ulivyo. Umekuwa unaiga mambo ya wengine na kutaka maisha yako yawe kama ya watu wengine. Kwa kukazana kufanya hivi unasahau lengo lako muhimu kwenye maisha na hivyo kujikuta unakimbiza kila lengo linalotokea mbele yako. Ukiona mtu kanunua kitu na wewe unataka ununue, sio kwa sababu unahitaji, bali kwa sababu na wewe unataka usibaki nyuma.
Wakati mwingine unajikuta unalazimika kuishi maisha ambayo sio unayopenda kwa sababu tu jamii nzima inaishi hivyo. Imekuwa ni kawaida kwa jamii kutupangia ni jinsi gani tutakavyoishi, ni kazi au biashara gani tunaweza kufanya na hata maisha tunayoishi. Kwa kutaka kwenda na jamii kwenye hali hii ndio kunasababisha maisha yanakuwa magumu sana kwa sababu hufanyi kile ambacho kinatoka moyoni mwako na hivyo unakosa furaha.

SOMA; Wajue Watu Hawa Wanaokazana Kukurudisha Nyuma Na Jinsi Ya Kuwashinda.


Amua sasa kushika hatamu ya maisha yako, amua kufanya kazi au biashara unayopenda, amua kuishi maisha ambayo utayafurahia. Tuna muda mfupi sana wa kuwepo hapa duniani, tafadhali usiupoteze kwa kuishi maisha ambayo huyafurahii. Ishi maisha ambayo yataleta tofauti kwako na kwa wale wanaokuzunguka, na hata ukiondoka utaacha alama.

TAMKO LA LEO;
Najua sehemu kubwa ya ugumu wa maisha yangu nasababisha mwenyewe, kwa kujaribu kuishi maisha ambayo sio yangu, kwa kutaka kufanya kile ambacho kila mtu anafanya na kwa kulazimika kuishi kama vile ambavyo jamii inataka niishi. Kuanzia sasa nakataa maisha ya aina hii, na nitaishi yale maisha ambayo nayapenda na yataleta tofauti kwangu na kwa wanaonizunguka.

Tukutane kwenye ukurasa wa 151 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Friday, May 29, 2015

#NENO_BUSARA; Tatizo La Vitu Ambavyo Ni Rahisi Kufanya.

Tatizo la vitu ambavyo ni rahisi kufanya ni kwamba ndio vitu ambavyo ni rahisi kutokufanya.
Ni rahisi sana kuwa na afya bora, kwa kula vyakula bora, mboga mboga na matunda. Lakini pia ni rahisi sana kutokula vyakula hivyo, kutokana na wingi wa vyakula visivyo vya afya.
Ni rahisi sana kufikia uhuru wa kifedha. Nunua kile unachohitaji kutumia tu, punguza matumizi yasiyo ya lazima na wekeza angalau sehemu ya 10 ya kipato chako. Lakini pia ni rahisi kutokufanya hivi, kwa sababu kuna vitu vizuri na vya kuvutia, ambavyo vinatamanisha kununua, japo sio muhimu kwako. Na hata kama huwezi kulipia unaweza kukopeshwa na hivyo kujikuta kwenye shimo refu la madeni na matatizo ya kifedha.
Ni rahisi sana kufanikiwa, chagua kile unapenda kufanya na weka moyo wako wote kwenye kukifanya. Lakini pia ni rahisi sana kutokufanikiwa, kwa sababu kuna vitu vingi vizuri vya kufanya na pia huna muda wa kutosha kuweka moyo wako wote kwenye kile unafanya. Na hapo bado watu hawajakukatisha tamaa kwa kukuambia huwezi au haiwezekani.
Vitu ambavyo ni rahisi kufanya ndio vitu ambavyo ni rahisi kutokufanya. Jua hili na uchukue hatua.

Ukurasa Wa 149; Hawa Ndio Watu Unaotakiwa Kuwafikiria Zaidi.Utakapoamua kuboresha maisha yako, utakapoamua kufanya tofauti na ulivyokuwa unafanya na utakapoanza kupata majibu ya tofauti na uliyokuwa unapata mwanzo, kuna watu watakuchukia. Nataka nikuambie hilo wazi. Kuna watu watakuchukia wazi wazi na kukuambia huwezi au unapoteza muda wako, na hata ukiweza watakuambia subiri. Na kuna wengine watakuchukia kwa ndani bila ya wewe mwenyewe kujua, ila utaona wamepunguza ushirikiano na wewe.

SOMA; Haya Ndio Makundi Matatu Ya Watu, Je Wewe Upo Katika Kundi Lipi?

Habari nzuri ninazotaka kukupa pia ni kwamba kwa kuamua kufanya hivi kuna watu ambao watakupenda. Kuna watu watafurahia jinsi maisha yako yamebadilika, kuna watu watapenda thamani uliyoongeza na wataendelea kuwa na wewe.
Sasa ni watu wapi ambao atakunyima usingizi, ni wapi ambao utawafikiria zaidi? Kwa hali ya kawaida ya kibinadamu utawafikiria sana wale ambao wanakuchukia au wanakupinga. Ukifikiria ni njia gani unaweza kutumia ili kuwaonesha kwamba wewe ni zaidi ya wanavyofikiria. Kuwaonesha kwamba hawakujui vizuri. Unaweza kufanya hivi ila nataka nikuambie kwamba utakuwa unapoteza muda wako bure. Watu ambao hawakukubali sasa, hawatakukubali milele au huenda itawachukua muda mrefu kufanya hivyo, chochote utakachofanya, watatafuta njia ya kuona kwamba bado huwezi.
 
SOMA; Hiki Ndio Kitu Kikubwa Unachohitaji Kufanya Ili Kuboresha Maisha Yako(Zawadi Yangu Kwako).
Tumia muda wako mwingi kuwafikiria wale ambao wanakukubali na kupenda kile unafanya. Watu hawa wakunyime usingizi ukifikiria ni jinsi gani unaweza kuwaboreshea zaidi kile wanachokipenda na kwa njia hii utawanufaisha zaidi na wao watakunufaisha zaidi na pia watakuletea wengi zaidi wa aina kama yao.
Ukitumia muda mwingi kuwafikiria wale ambao wanakuchukia na kukupinga, unawadhulumu wale ambao wanakupenda na kukuhamasisha. Muda ni mfupi sana kuanza kuhangaika na watu ambao hawajali na hawatojali, fanya kazi na wale wanaojali, na utakuwa na maisha yenye furaha na mafanikio.
TAMKO LA LEO;

Muda wangu ni mfupi sana siwezi kuutumia kuwafikiria wale ambao wananichukia na kunipinga. Nitatumia muda huu kuwafikiria wale wanaonipenda na kunikubali. Nitaendelea kufanya kile ninachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana kwa sababu najua ndio kitakachoniletea mafanikio na furaha kwenye maisha yangu.

Tukutane kwenye ukurasa wa 150 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.