Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Showing posts with label FIKRA MBADALA. Show all posts
Showing posts with label FIKRA MBADALA. Show all posts

Friday, January 23, 2015

JICHO KWA JICHO; Tutabaki Na Dunia Ya Vipofu.

Kama tunakubaliana ni JICHO KWA JICHO basi tukubaliane kwamba dunia nzima tutabaki vipofu.

Kama tunakubaliana ni JINO KWA JINO, tukubali pia kubaki vibogoyo dunia nzima.

Kama tutakubaliana UPANGA KWA UPANGA pia tujiandae kwa mafuriko ya damu duniani.

Tukisema CHUKI KWA CHUKI tujiandae kuishi dunia yenye simanzi kubwa.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

Kama ilivyo kwamba giza haliwezi kuondoa giza, bali mwanga ndio unaondoa giza.

Ndivyo ilivyo kwmaba chuki haiwezi kuondoa chuki, bali upendo ndio utaondoa chuki.

TUPENDANE.

SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.

Saturday, January 3, 2015

Nilichojifunza Kwa Panya Road Na Kwa Nini Tutaendelea Kuwa Masikini Kwa Miaka Mingi Ijayo.

Jana tarehe 02/10/2015 kulikuwa na tafrani kubwa sana katika maeneo mengi ya jiji la dar es salaam. Tafrani hii ilisababishwa na kikundi cha vijana wanaojiita panya road ambao ni genge la uhalifu linalovamia watu na kupora mali kwa kutumia silaha mbalimbali ambazo sio za moto.

Hofu ya uvamizi wa vijana hao kwa jana ilisambaa kwa kasi sana kwenye maeneo mengi ya dar. Uvamizi ulifanyika maeneo machache ila athari za hofu zilisambaa kwenye maeneo mengi na kuleta matatizo mengi.

Katika eneo ninalokaa, tabata, hofu hii ilifika kwa kasi sana na watu walianza kukimbia hovyo, maduka na bar zilifungwa na bara bara zilibaki nyeupe. Waendesha pikipiki maarufu kama boda boda walikuwa mshari wa mbele kusambaza hofu hii. Kwani walikuwa wanapita mitaani wakikimbiza piki piki na kuwaambia panya road wako karibu na wanakuja.

Kwa kweli lilikuwa ni tukio la ajabu sana hasa ukiangalia wingi, nguvu na hata silaha wanazotumia vijana hawa na jinsi hofu hii ilivyowaathiri wengi.

Najua kila mmoja sasa hivi analaani kitendo hiki, kila mmoja analaumu jeshi la polisi kwa uzembe na kila mmoja anajiuliza serikali inashindwaje kudhibiti kikundo cha vijana wanaotumia mapanga, visu, nyembe na mawe.

Wakati hayo yakiwa ya msingi kufikiria, mimi nimejifunza mambo machache kutokana na tukio hili na mambo haya nashawishika kwamba yatatufanya tuendelee kuwa masikini kwa miaka mingi ijayo.

Jambo la kwanza; Watu ni waoga sana na hofu ni mbaya mno.

Wakati tunapata taarifa hizi watu walikuwa wanakimbia hovyo, maduka na bar vinafungwa na kila mtu alikuwa na heka heka. Muda kidogo tukapata taarifa maeneo mengine kama matano hali ni hiyo hiyo. Sasa nikafikiria hawa vijana wako wangapi kiasi kwamba waweze kuteka magomeni mpaka ubungo mpaka mabibo mpaka tabata kwa wakati mmoja. Kikubwa kilichokuwa kinaendelea ni hofu.

Nilishuhudia mama mmoja anaacha gari na kukimbia kwa miguu, hapo hakuna aliyeona sura ya hao panya road bali ni taarifa tu za uwepo wao.

Hofu hii tuliyoishuhudia kwenye sakata hili la panya road ndio inatufanya tuendelee kuwa masikini. Ni hofu hii inawafanya wengi kuendelea kufanya kazi ambazo hawazipendi na haziwapatii kipato cha kutosha ila kwa hofu kwamba nikiacha kazi hii nitafanya nini wanajikuta wanakubali kuwa watumwa.

Ni hofu hii ambayo inawafanya watu kuogopa kujarimu mambo mapya, kuogopa kuzijaribu fursa mpya zilizopo mbele yao na kung’ang’ania kufanya kile walichozoea kila siku ambacho hakiwazalishii kiasi cha kutosha.

Ni hofu hii hii ambayo inatufanya tuogope kudai haki zetu hata pale zinapovunjwa wazi wazi. Tukiamini kwamba iko siku mambo yatakuwa mazuri na hatimaye maisha yetu kuwa hovyo kila siku zinavyokwenda.

Jambo la pili; Watu ni wabinafsi sana.

Katika sakata hili nilishuhudia kitu kimoja ambacho kiliniumiza sana. Kuna wamama ambao walijifungia saluni na wakati huo akaja mtoto mwenye umri kama wa miaka sita amembeba mdogo wake mgongozi. Mtoto yule akawa anawaomba wamama wale wamfungulie aingie lakini hawakudhubutu kufanya hivyo. Mtoto alibaki nje akilia kwa hofu kubwa iliyokuwa imetanda.

Kama watu wote waliokuwa wanakimbia hovyo wangeacha kujiangalia wao binafsi na wakakaa pamoja sidhani kama kikundi hiki kingeweza kuleta tafrani kubwa kiasi hiki. Kitendo cha kila mtu kujijali yeye zaidi kilitoa nafasi kubwa ya hofu kuendelea kusambaa kwa wengine.

Ubinafsi huu kama taifa unatufanya tuendelee kuwa masikini kwa kipindi kirefu kijacho. Ni ubinafsi huu unasababisha watu wachache kuwa mafisadi wakubwa. Ni ubinafsi huu unaotumika kuwagawa wanaopigania haki na hatimaye kushindwa.

Tunahitaji kupambana na matatizo haya makubwa mawili, hii inahitaji kuanzia kwa kila mwananchi mpaka kwa viongozi.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Tuesday, December 30, 2014

Kama Hutofanya Chochote…

Kama hutofanya chochote hakuna kitakachotokea…

Kama ukifanya chochote, chochote kinaweza kutokea…

Ndio unaweza kuishia huna kitu, lakini hapo ndio ulipoanzia.

Una nini cha kupoteza?

Fanya kitu kubadili maisha yako sasa.

Monday, December 29, 2014

Hiki Ndio Kitakachotokea Miaka 100 Ijayo..

Sio kwamba nimekuwa mtabiri ila nina uhakika miaka mia moja ijayo kitu hiki kitatokea.
Kitu hiko ni kwamba wote tunaosoma hapa tutakuwa tumekufa. Ndio namaanisha hata wewe utakuwa umekufa miaka mia moja ijayo kuanzia leo, yaani mwaka 2114.
Na kwa bahati nzuri sana tutakuwa tumekufa kwa kipindi kirefu sana, kwa miaka zaidi ya trilioni inayokuja tutakuwa tumekufa.
Nakwambia yote haya ili nini, si unayajua?
Nataka ufanye nambo mawili;
1. Ishi maisha yako kwa furaha maana muda unaoishi ni mfupi kuliko ambao utakuwa umekufa.
2. Hakikisha unagusa maisha ya wengine ili utakapoondoka uache kumbukumbu ya kuwepo kwako. Kujua jinsi ya kufanya hivyo soma makala hii; sio wote tunaowazika wamekufa.
Kila la kheri.

Sunday, December 21, 2014

Ishi na Waache wengine nao waishi...

Ishi na waache wengine nao waishi,
Fanya biashara na waache wengine nao wafanye biashara,
Vua samaki na waache wengine nao wavue samaki,
Kula raha na waache wengine nao wale raha...
Kuna fursa nyingi sana hapa duniani hivyo hakuna haja ya kiwabania wengine.
Kama ilivyo kwamba huweza kulinda bahari na kusema ni yako, ndivyo ilivyo kwa fursa.
Nakutakia kila la kheri.

Saturday, December 20, 2014

Hawa Ndio Watu Unaoishia Kuwa Nao...

Unaishia kuwa na watu ambao unawavumilia...
Marafiki ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye tabia ambazo unazivumilia na hakuna aliyekulazimisha uwe nao.
Wafanyakazi ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye ufanisi ambao unauvumilia na hakuna aliyekulazimisha kuendelea kuwa nao.
Wateja ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye tabia ambazo unazivumilia na hakuna aliyekulazimisha kuendelea kuwa nao.
Mwajiri uliyenaye ni yule unayemvumilia, mwenye tabia unazozivumilia na anayekupa kipato unachokivumilia, hakuna aliyekulazimisha uendelee kuwa naye...
Yote hii ina maana gani?
Maana kubwa ni kwamba MAISHA NI UCHAGUZI, unachagua nani awe rafiki yako, nani awe mwajiri wako, nani awe mfanyakazi wako na nani awe mteja wako.
Kama kuna ambaye unaona hafai kuwa mmoja kati ya hao, unamfukuza, unaachana nae na kujumuika na yule unayeendana nae.
Maisha yako, uchaguzi wako.

Friday, December 19, 2014

Wewe Ni Wa Kwanza Kusoma Hapa…

Ndio wewe ni wa kwanza kusoma hapa, yaani ndio unapata habari hii kwa mara ya kwanza na unaipata hapa tu.

Wewe ni wa kwanza kusikiliza wimbo huu mpya, na unausikia kwa mara ya kwanza kwenye kituo hiki cha redio tu.

Wewe ni wa kwanza kupata habari hizi mbaya za ajali, umezisikia hapa tu…

Kuwa wa kwanza kupata kila habari inayotokea, kila linalofanyika, masaa 24 kwa siku, siku saba bkwa wiki.

Swali; je ukishakuwa wa kwanza inabadilisha nini?

Kupenda kuwa wa kwanza kwa vitu ambavyo havina msaada mkubwa kwentu kunatufanya tushindwe kufuatilia yale ambayo ni ya muhimu kwetu.

Kwa mfano unasoma kwenye mtandao; mtu fulani maarufu amekufa, na wewe kwa kuwa unataka kuwa wa kwanza kutoa habari, unakimbilia kusambaza, bila hata ya kudhibitisha kweli kama amekufa.

Wednesday, December 17, 2014

Mabadiliko Yanaanzia Hapa...

Mabadiliko yanaanza na yule anayetaka mabadiliko...
Kama unataka watu wakuheshimu anza wewe kuwaheshimu...
Kama unataka watu wakupende anza wewe kuwapenda...
Kama unataka watu wafanye unachotaka anza wewe kufanya kitu hiko.
Ni vigumu sana kumlazimisha mtu afanye kile unachomtaka afanye.
Ila ni rahisi sana mtu kuiga kile unachofanya.
Badala ya kupoteza nguvu nyingi kumwambia mtu kwa nini abadilike, kwa nini usoelekeze nguvu hizo katika kuanzisha mabadiliko yenyewe?

Hili Ndilo Kaburi Unalozika Ndoto Zako Kubwa.

Jana ulipanga leo utaanza kuweka mipango ya kuanza biashara,
Au ulipanga leo utaanza mazoezi,
Au ulipanga leo utaanza kuweka akiba ya kila unachopata,
Au ulipanga utaboresha kazi yako zaidi...
Leo imefika, unajikumbusha kwamba unahitaji kufanya ulichopanga jana, lakini mwili haupo tayari kabisa kufanya.
Nafsi inaanza kukusuta, ulipanga leo utafanya, mbona hufanyi? Kwa haraka linakuja wazo linalotuliza nafsi yako.... NITAFANYA KESHO....
Baada ya wazo hili unaacha kujisuta na kukubali kwamba kesho mambho yataanza rasmi.
Na kweli kesho mambo yanaanza rasmi kweli, ila ni mambo kama uliyofanya leo, kusema utaanza kesho.
NITAANZA KESHO ni kaburi la ndoto kubwa sana. Ndoto nzuri na za kuboresha maisha yako umezizika kwenye kaburi hilo.
Acha sasa kuzika ndoto zako, kama kuna kitu muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako, kifanye sasa, sio kesho.

Friday, December 12, 2014

Msitu Msituni…

Ukiwa mbali na msitu, yaani kabla hujaingia msituni utauona msitu ni mkubwa sana. Utaona eneo lote la msitu limejaa miti na huwezi kuona hata ardhi. Kwa umbali uliopo unaweza kuamini kwamba hakuna hata sehemu ya kupita kwenye msitu huo.

Ila unapoingia kwenye msitu huo, huoni tena msitu. Yaani unapokuwa msituni huoni tena msitu, bali unaona mti mmoja mmoja na kuna sehemu kubwa ya kupita. Unaweza kuupita mti mmoja baada ya mwingine na kuendelea kufanya yako…

Kabla hujaingia kufanya jambo lolote utaona vikwazo vingi sana, utaona hatari na ilivyo rahisi kushindwa. Ila unapoingia kwenye jambo hilo, vikwazo vilivyokuwa vinakutisha mwanzo unakuta sio vikubwa kama ulivyokuwa unafikiri. Unakuta ni changamoto ndogo ndogo ambazo unaweza kuzimudu.

Usiogope tena kufanya kile unachotaka kufanya, huwezi kuona msitu ukiwa msituni…

Nakutakia kila la kheri.

Wednesday, December 10, 2014

Waliofika kileleni…

Watu waliofika kwenye kilele kikubwa sio kwa sababu watu hao waliruka na kujikuta kileleni, ila kwa sababu watu hao, wakati wenzao wamepumzika wao waliendelea kukomaa na kuendelea na safari.

Endelea na safari yako wakati wengine wamelala…

Endelea na safari yako wakati wengine wanastareheka…

Endelea na safari yako wakati wengine wanabishana mambo ambayo hawawezi kuyaathiri…

Watakuona upo kileleni, wakati wao wakiendelea kusota na kushindwa kufika kwenye kilele.

Tuesday, December 9, 2014

Ana Miaka 53 Ila Bado Analishwa Uji…

Kwa kawaida mtu yeyote anayezaliwa huwa anapitia vipindi tofauti kwenye maisha yake.

Kwanza kabisa anaanza kama mtoto ng’aa, ambapo anakuwa anategemea kunyonya maziwa ya mama tu.

Anaendelea kukua na baadae anakuwa analishwa uji, huku akikazana kutambaa na hatimaye kutembea.

Baada ya muda anaanza kula matonge ya ugali na kukimbia mwenyewe..

Baadae kabisa anakuwa mtu mzima anayejitegemea na kuweza pia kuwasaidia wengine.

Mpaka kufika miaka 53, mtu anatakiwa awe ameshapitia vipindi vingi vya ukuaji na maendeleo kwa ujumla. Na huu ndio umri ambao anakuwa ameshakamilisha mambo mengi kwenye maisha yake na anaishi maisha ya furaha.

tz1

Sasa maajabu makubwa ni pale unapomkuta mtu mwenye miaka 53 bado analishwa uji. Yaani yeye tokea atoke kwenye hatua ya kwanza ya kunyonya amekwamba kwenye hatua ya pili ya kunyweshwa uji.

Kama akitishiwa kunyimwa uji huo anaolishwa anaanza kulia sana na kuona maisha yake yatakuwa magumu.

Sio kwamba mtu huyu alizaliwa na ulemavu wa aina yoyote, na wala sio kwamba amekosa nguvu au mbinu nyingine za kujitegemea, yeye amefurahia kulishwa uji na hataki kufikiria zaidi ya hapo.

Ni jambo la kushangaza sana unapomkuta mtu mzima, miaka 53, mwenye afya na nguvu akiendelea kulishwa uji…

Monday, December 8, 2014

Nyasi Za Upande Wa Pili Ni Za Kijani Zaidi…

Angalia zile nyasi za upande wa pili, ni za kijani zaidi ya nyasi zilizopo upande wako…

Hii ni fikra ambayo huwa inamjia kila mtu katika sehemu aliyopo iwe ni maisha, kazi au biashara.

Unaweza kuona wenzako wana maisha mazuri kuliko hayo uliyoko nayo kwa sababu tu unaona wanatembelea magari mazuri au wanaonekana sehemu nzuri nzuri…

Unaweza kuona kazi au biashara wanazofanya wengine ni nzuri na zinawalipa zaidi kuliko kazi au biashara unayofanya wewe…

nyasi

Hii sio kweli kabisa, unaziona nyasi hizo ni za kijani zaidi ya za upande wako kwa sababu hujafika kwenye nyasi hizo. Utakapo pata nafasi ya kufika kwenye nyasi hizo utagundua kwamba hazina tofauti kubwa na nyasi zako.

Thamini kile ulicho nacho na kama unataka kiwe bora zaidi, kiboreshe. Usiyumbishwe kwa kutamani wanayofanya wengine, huenda hata wao wanatamani unayofanya wewe.

Hivyo njia bora sio kuangalia nyasi zipi ni za kijani zaidi, bali zifanye nyasi zako kuwa za kijani zaidi.

Nakutakia kila la kheri.

Sunday, December 7, 2014

Tulikuona Wakati Unakuja Mjini…

Tulikuona wakati unakuja mjini, usijione mjanja leo…

Ulikuja umevaa yeboyebo na nguo umebeba kwenye mfuko wa rambo, leo unajiona unajua sana…

Hayo ni maneno ya hovyo sana yanayotolewa na watu walioshindwa. Watu ambao wamepoteza muda wao kwa kufikiri wao ni wakongwe na anakuja mtu na kuwaacha wakishangaa.

Ili kujifariji kwamba na wao wana kitu fulani wanatumia sababu hiyo ya ukongwe.

joti-mpoki-enzi-hizo

Sikiliza mafanikio hayapimwi kwamba ulizaliwa wapi au umekulia wapi. Mafanikio yanapimwa na nini unachoweza kuonesha watu kwamba umefanya na kimeleta mabadiliko kwenye maisha ya wengine.

Kama wewe ndio unaambiwa wakuja usihofu, endelea kukazana.

Kama wewe ndio unawaambia wenzako ni wakuja soma hapa; ONDOKA NYUMBANI. Itakusaidia sana na utajua ni hatua gani ya kuchukua.

Chukua hatua sasa…

Saturday, December 6, 2014

Bado Hujachelewa...

Kuna bwana mmoja alikuwa analalamika ni jinsi gani alikuwa anapenda kujifunza kupiga kinanda ila akakosa muda kwenye maisha yake.
"Kwa nini usianze sasa" rafiki yake alimuuliza.
"Unashangaza wewe" yule bwana alimjibu. "Nina miaka hamsini sasa, nikianza kujifunza leo itanichukua miaka mitano mpaka nijue kupiga kinanda vizuri, wakati huo nitakuwa na miaka hamsini na tano" aliongeza bwana yule.
Rafiki yake alimsikiliza kwa makini kisha akamuuliza, " kama usipoanza kujifunza kinanda leo, miaka mitano ijayo utakuwa na miaka mingapi"?
Katika simulizi hii fupi unaweza kuona ni jinsi gani tunajijengea vikwazo visivyo na msingi sisi wenyewe.
Kama kuna jambo lolote unalotaka kufanya kwenye maisha yako bado hujachelewa kulifanya, ANZA SASA...
Nakutakia kila la kheri,
Kama unahitaji ushauri wa kina juu ya jambo lolote linalokusumbua andika email kwenda ushauri@kisimachamaarifa.co.tz
Karibu sana.

Tunarudia Makosa Yale Yale…

Hakuna makosa mapya, tunarudia makosa yale yale.

Ila kwa kuwa teknolojia imekua basi na kiwango chetu cha kufanya makosa yale yale tuliyokuwa tunayafanya zamani kimebadilika.

Watu wamekuwa wakiambiwa wasiue zaidi ya miaka 4000 iliyopita sasa, lakini mpaka leo bado wanaua.

Usiibe, usizini, bado kila siku tunarudia makosa haya haya.

Hii ni kwa sababu sisi ni binadamu, na tunakosea kila mara. Lakini hii haituzuii kuwa bora zaidi ya tulivyo sasa. Tunaweza, tufanye.

Friday, December 5, 2014

Mwalimu Anakusubiri, Chukua Hatua Sasa…

Mwanafunzi anapokuwa tayari mwalimu hutokea…

Huu ni usemi wa kale kidogo ila unaobeba maana kubwa sana.

Mwanafunzi anapokuwa tayari mwalimu hutokea, sio kwa sababu mwalimu alikuwa anasubiri mwanafunzi awe tayari ndio ajitokeze bali mwalimu alikuwepo muda wote ila mwananfunzi anapokuwa tayari ndio anamuona mwalimu kuwa yupo.

Mambo mengi kwenye maisha ambayo hujayawekea mkazo huwezi kuona umuhimu wake, pale unapoyawekea mkazo ndio unaona umuhimu wake na ndio unaona fursa zaidi.

Hivyo kuwa tayari ili uweze kumuona mwalimu wako na unufaike zaidi.

Walimu wapo wengi na kwa uhakika tu walimu wafuatao wanakusibiria wewe uwe tayari ili waanza kukupa yale kuhimu;

AMKA CONSULTANTS

AMKA MTANZANIA

KISIMA CHA MAARIFA

UWEKEZAJI TANZANIA

Hiyo ni baadhi ya mitandao ambayo utajifunz amambo mengi sana kuhusu mafanikio na maisha kwa ujumla.

Chukua hatua sasa, mwalimu anakusubiri.

Thursday, December 4, 2014

Hii Ndio Ardhi Yenye Utajiri Mkubwa Sana Duniani.

Kuna ardhi yenye utajiri na thamani kubwa sana duniani...
Ardhi hiyo sio yenye visima vya mafuta..
Na wala sio ardhi yenye migodi ya madini...
Bali ardhi hiyo ni makaburi,


Makaburi yamejaa ndoto nyingi sana ambazo hazikutimizwa.
Kuna mawazo makubwa ya kibiashara ambayo hayakutimizwa...
Kuna mawazo na ndoto kubwa za mabadiliko ambazo hazikupata nafasi ya kutekelezwa.
Badala yake watu hawa walikufa na ndoto zao.
Angalia na wewe usijekufa na ndoto yako kabla hujaitekeleza,
Maana utainyima dunia kitu kizuri sana.

Wednesday, December 3, 2014

Lazima Wakufanye Uendelee Kuwa Mjinga...

Ili uendelee kuwaona wao ni muhimu ni lazima waendelee kukufanya wewe mjinga...
Kwa sababu ukijua wanavyojua hutaona umuhimu wao tena...
Huu ndio ukoloni mpya unaoathiri sehemu kubwa ya watu..,
Kudai uhuru wako, unajua cha kufanya.

Tuesday, December 2, 2014

Aina Mbili Za Ujinga.

Kuna aina mbili za ujinga, kulingana na uelewa wa mjinga mwenyewe.
Kuna ujinga wa juu juu ambapo mtu hajui lakini anafikiri kuna mtu anajua.
Na kuna ujinga wa kweli ambapo mtu hajui na anajua hakuna anayejua.
Wanafunzi wana ujinga wa juu juu,
Wataalamu wana ujinga wa kweli.
Hii ndio inatufanya tuwe na kiu ya kutafuta kujua zaidi na hivyo kujifunza zaidi.