Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Thursday, July 2, 2015

UKURASA WA 183; Hakuna Anayekuchukia Wewe, Bali Wanahamisha Chuki Zao Kutoka Hapa.

Leo naomba tujadili kidogo kuhusu mtu kumchukia mwingine.
Labda tuseme wewe kuna mtu anakuchukia, na amekuwa akikuonesha wazi wazi kwamba anakuchukia. Na hapa wewe huna tatizo lolote na mtu huyu. Unajaribu kuishi maisha yako bila hata ya kuingilia maslahi yao wala kuwavurugia chochote ambacho ni chao, lakini mtu anachagua tu kukuchukia.
Unajisikiaje katika hali kama hii? Unaumia kwa sababu ulitegemewa mtu ambaye ni wa karibu kwako awe pamoja na wewe badala yake anakuchukia? Unajaribu kumbadili mtu labda akupende?
Leo nataka nikupe sababu kwa nini mtu anaweza kukuchukia na njia bora ya kuondokana na chuki hiyo.
Kwanza kabisa mtu anapokuchukia sio kwamba anakuchukia wewe, ila anajichukia yeye binafsi. Ni hivyo tu. Mtu kuna kitu ambacho kinamsumbua kwenye maisha yake na hataki kukikubali, hivyo anayachukia maisha yake, kwa sababu hataki kukubali hilo pia anatafuta mtu wa kumchukia ili angalau aone tatizo sio lake. Si unajua tabia za wakwepa majukumu?
Hivyo atajipa kila sababu kwa nini anakuchukia wewe, lakini wewe huna tatizo lolote na yeye kukuchukia, hakuna chochote ambacho umemharibia. Labda umeamua tu kubadili maisha yako na kwa kuwa huyo anayekuchukia hawezi kubadilika basi anakuchukia. Kwa mfano ulikuwa na marafiki wa karibu kila siku mnakunywa pamoja, wewe ukakaa chini na kuona kunywa kwenu hakuna faida yoyote, hivyo ukaamua kuacha utaratibu huu wa kukutana baa kila siku na ukaanza kujifunza na kujishughulisha na vitu vya pembeni(fanya hivi kama bado una utaratibu wa kuhudhuria vikao vya baa kila siku). Unafikiri ni nini kitatokea kwa marafiki zako hao? Watakuchukia. Sasa hebu jiulize wanakuchukia kwa sababu wewe umeamua kuacha kukaa vikao hivyo kila siku? Hapana, wanakuchukia kwa sababu wewe unaanza kuwa bora kuliko wao. Kwa mfano ingetokea huna tena kazi na hivyo huna fedha ya kwenda baa kila siku unafikiri wangekuchukia? Hawawezi kukuchukia, watakuonea huruma tu na wataendelea na utaratibu wao.
Hivyo kama kuna mtu yeyote ambaye anakuchukia, wala usijiumize kichwa ufanye nini ili aache kukuchukia, endelea kufanya unachofanya na mwache ajiue mwenyewe na chuki zake. Maisha ni mafupi sana mpaka uanze kupata muda wa kumfurahisha kila mtu.
Usikubali uhusiano wowote wa kindugu au kirafiki uwe kikwazo kwako kuishi maisha unayotaka kuishi wewe, kama huvunji sheria. Hata kama kuna atakayekuchukia hawezi kukuchukia zaidi ya miaka 100 ijayo, kwa sababu wote mtakuwa mmekufa na hakuna atakayekuja kukukumbusha kwamba nilikuchukia sana duniani, kama mtakutana peponi.
SOMA; Hiki Ndio Kitakachotokea Miaka 100 Ijayo..
Maisha ni yako chaguo ni lako, kama kuna mtu anakuchukia muonee huruma na achana naye, wala hata usimfikirie, wewe endelea kuweka juhudi kwenye kile unachofanya na unachotaka kuwa bora.
TAMKO LA LEO;
Najua kwamba mtu yeyote anayenichukia sio kwa sababu ananichukia kweli, ila ni kwa sababu anajichukia yeye mwenyewe. Mimi sina muda wa kuanza kufikiria kuhusu anayenichukia, ni bora nikatumia muda huo vizuri kujiendeleza kuwa bora zaidi kwenye hiki ninachofanya.
Tukutane kwenye ukurasa wa 184 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Tafadhali Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri!
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →
Powered By: BloggerYard.Com

0 comments:

Post a Comment