Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Thursday, June 18, 2015

UKURASA WA 169; Utaendelea Kuidhulumu Dunia Mpaka Lini?


Kila mmoja wetu ana kitu kikubwa sana ambacho kipo ndani yake, ambacho akikitoa anaweza kuleta mabadiliko makubwa sana kwa watu wengine. Lakini tatizo kubwa ni kwamba wengi wetu hatutoi vitu hivi. Na tumekuwa tunaidhulumu dunia kwa kiasi kikubwa sana.
Kazi ambayo nimekuwa naifanya, ya uandishi na kufundisha, imekuwa inawasaidia watu wengi sana. Najua hili kwa sababu wengi wamekuwa wakiniandikia jinsi ambavyo maisha yao yanabadilika. Wakati naanza kuandika, nikiwa bado nakazana kutafuta njia gani ya uandishi ninaipendelea na nitapata watu wa kunisikiliza na kufanyia kazi kile ninachoandika, kuna wakati niliona hakuna kikubwa kwenye uandishi huu, nafanya kwa sababu napenda tu kuandika. Ila kwa sasa, kama nikisema niache kuandika leo, nitakuwa nimefanya dhuluma kubwa sana kwa dunia hii. Ni jukumu langu kuendelea kutoa maarifa ambayo yanawawezesha watu kubadili maisha yao, na kuyafanya yawe bora zaidi ya yalivyokuwa hapo awali.
Hata wewe pia una kitu kikubwa cha kutoa kwenye dunia hii. Kupitia biashara au kazi unayofanya, usiangalie tu ni mshahara kiasi gani unapata, usiangalie tu ni faida kiasi gani unapata, angalia ni thamani gani unatoa kwa wengine. Angalia ni jinsi gani unayagusa maisha ya wengine. Fanya hivi kwa moyo mmoja na kwa juhudi kubwa na ninakuhakikishia, ndio nakuhakikishia kwamba dunia italazimika kukulipa, na itakulipa kwa kiwango kikubwa sana mpaka mwenyewe utashangaa muda wote ulikuwa wapi hukulijua hili.
SOMA; Vitu Ambavyo Ni Rahisi Kufanya.... Na Madhara Yake.
Wewe ni mwandishi? Andika mpaka mtu ashawishike kufanya kile unachoamini ni sahihi kwake kufanya, na atakapofanya na akafanikiwa, atakulipa, kwa kiwango kikubwa sana.
Wewe ni muimbaji? Imba mpaka watu wasimame, watu waache kufanya wanachofanya wakusikilize, watu watafute wimbo wako wakati wanajisikia kukata tamaa, na wautafute pia wakati ambapo wana furaha na watakulipa sana.
Wewe ni mwalimu? Fundisha mpaka watu waelewe, hakikisha hakuna anayetoka akiwa mtupu na hata kama haelewi lile somo unalomfundisha basi hakikisha unamfundisha chochote kitakachomsaidia kwenye maisha.
Wewe ni daktari? Toa huduma nzuri za afya zitakazookoa na kuboresha maisha ya watu. Fanya kila unachoweza kuhakikisha kwamba mgonjwa anayekuja kwako akiwa amekata tamaa kwamba maisha yake ndio yanafika tamati, aondoke akiwa na maisha yenye matumaini, hata kama huwezi kumponesha, basi umpunguzie hata maumivu. Na dunia italazimika kukulipa.
Hakuna kitu kizuri ambacho utakifanya na dunia ikaacha kukulipa, nina uhakika na hili. Nakusihi sana, fanya leo. Hata kama ni mzazi, toa malezi bora kwa mtoto wako na wanaokuzunguka pia, dunia itakulipa.
TAMKO LA LEO;
Najua nimekuwa naidhulumu dunia kwa kushindwa kutumia uwezo mkubwa ambao upo ndani yangu. Kuanzia sasa nitafanya kile ninachofanya kwa moyo mmoja na kwa ajili ya kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Najua dunia itanilipa kwa hili na fedha haitakuwa tatizo kubwa kwangu. Kila siku nitaikopesha dunia kwa kufanya mambo ambayo ni bora na najua dunia italazimika kunilipa.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.

Tafadhali Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri!
SOCIALIZE IT →
FOLLOW US →
SHARE IT →
Powered By: BloggerYard.Com

0 comments:

Post a Comment