Enzi zangu mimi bwana, hela ndogo ndogo kama hizi zilikuwa hazinipigi chenga.....
Enzi hizo nilikuwa msanii maarufu sana sema basi tu sasa hivi mambo yangu hayako vizuri...
Enzi zangu biashara niliyokuwa nafanya ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Sema sasa hivi tu mambo hayajakaa vizuri.....
Enzi hizo kazini mimi ndio nilikuwa kila kitu, ila hawa vijana wa siku hizi wamekosa heshima na kunichukulia mtu wa kawaida tu.....
Kama umeshaanza kutumia moja kati ya kauli hizo hapo juu nikupe pole kwa sababu umeshaondoka kabisa kwenye njia itakayokupelekea kwenye mafanikio. Ila nikupe moyo kwamba kama utasoma hapa na kama umekuwa unasoma makala nyingine kupitia mtandao huu basi una nafasi ya kubadili maisha yako.
Kauli hizo hapo juu ni dalili ya kukata tamaa, dalili ya kushindwa na dalili kwamba hakuna kitu kikubwa kinachoweza kutokea mbele yako. Kauli hizi zinatokana na mtu kufikia mafanikio fulani na kujisahau, kwa kujiona yeye ndio yeye n hivyo anaacha kujifunza na kuendelea kuweka juhudi. Baada ya muda mtu huyu anaachwa nyuma na kujiona kwamba hawezi tena.
SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.
Kama wewe ni mmoja wa watu hawa, napenda kukuambia kwamba anza leo kufanya tena kile ambacho ulikuwa unafanya. Acha mara moja kutumia kauli za enzi hizo na fanyia kazi kile ambacho unataka kuwa vizuri. Haijalishi una miaka 20 au 50 au 80 kama unajua kitu ambacho ulikuwa bora ila kwa sababu fulani ukajisahau, anza kukifanya tena. Anza kujifunza kuhusu kitu hiki, anza kuweka tena juhudi, weka ubunifu na usikate tamaa.
Kwa kufanya hivi utaanza kuona mabadiliko, utaanza kuona watu wakiheshimu tena vile viwango vyako na utarudi kwenye ngazi zako za mafanikio.
Acha kutumia kauli zinazoonesha kwamba jana yako ilikuwa bora kuliko leo, pambana kila siku inayokuja uwe bora zaidi kwenye kile unachofanya. Kama ilivyo kwa miti kwamba inaendelea kukua mpaka pale inapokufa, na wewe kuwa hivyo hivyo, endelea kukua kwenye biashara yako, endelea kukua kwenye kazi yako na endelea kukua kwenye kipaji chako bila ya kujali ni umri gani unao.
Siku utakayojiona kwamba wewe ndio unajua kila kitu, wewe ndio unaweza kila siku, hii ndio siku ambayo unajilaani mwenyewe na unaanza kurudi nyuma na kushindwa kufikia mafanikio makubwa zaidi.
TAMKO LA LEO;Tukutane kwenye ukurasa wa 169 kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kauli za enzi hizo ni kauli sumu kabisa kwangu kufikia mafanikio. Kuanzia sasa nitahakikisha kila siku nakuwa bora kuliko siku iliyopita. Sitaki nijisahau halafu nije kuona kwamba siku zilizopita nilikuwa vizuri. Nitajifunza kila siku, nitaweka juhudi kila siku na kila siku ya maisha yangu nitazidi kuwa bora kwenye kile ninachofanya. Najua hii ndio njia ya uhakika ya kufikia mafanikio.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment