Kuna vitu viwili muhimu sana unavyohitaji kuw anavyo ili uweze kufikia malengo na mipango uliyojiwekea na kufikia mafanikio makubwa. Vitu hivi viwili vinatoka ndani yako na vinaweza kukujenga au kukuangusha.
Vitu hivi viwili ni nidhamu na utashi.
Nidhamu tulishaijadili kwenye ukurasa wa nane. Kama hukupata nafasi ya kusoma kuhusiana na umuhimu wa kuwa na nidhamu ili kufikia mafanikio unaweza kusoma hapa; UKURASA WA 08; Nidhamu Ndio Nguzo, Ukiikosa Utaanguka.
Kitu kingine muhimu kitakachokuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa ua la ni utashi. Utashi ni ile hali ya kuweza kufanya maamuzi na kusimamia maamuzi hayo, yaani kuyatekeleza. Unapokuwa na malengo na mipango, haijitekelezi yenyewe, bali inahitaji wewe uifanyie kazi.
Ili kuifanyia kazi unahitaji kufanya maamuzi ya wewe kuanza kufanya kitu ili uweze kupata kile unachotaka. Huu ndio utashi, yaani nguvu ya akili yako kuamua kitu na kukisimamia.
SOMA; Kitu Hiki Kimoja Kitakufanya Uweze Kujiajiri, Uishie Kuwa Mwajiriwa Au Uishie Jela.
Unaweza kuona ni rahisi sana kwa kuamua tu ila sio rahisi kiasi hiko. Kwanza kabisa utashi wako unapungua kadiri muda unavyokwenda kwenye siku.
Kwa mfano unapoamka asubuhi unakuwa na nguvu kubwa ya utashi, unaweza kufanya mamauzi yoyote na kuyafanyia kazi. Lakini kadiri siku inavyokwenda nguvu yako ya utashi inapungua, ndio maana inapofika jioni unakuwa mvivu sana kufikiria na kuona umechoka. Inakuwa rahisi kwako kufanya vitu ambavyo havikuhitaji sana kufikiria kama kuangalia tv, kupiga soga na vingine vingi.
Sasa kuna makosa makubwa sana ambayo huwa tunayafanya kwenye matumizi ya utashi wetu. Makosa haya ni kuanza siku kw akufanya vitu ambavyo sio muhimu sana. Vitu hivi vinatumia nguvu yako ya utashi na kukuacha umechoka hivyo kushindwa kufanya mambo muhimu baadae. Kwa mfano unapoianza siku kwa kusoma email au kutembelea mitandao ya kijamii unaipa akili yako kazi nyingi ambazo sio muhimu. Baadae unapotaka kufanya kazi zako muhimu unajiona umechoka sana hivyo unasema nitafanya kesho. Kesho pia unarudia kosa hili hili na mwishowe unakuwa mtu wa kuahirisha mambo.
SOMA; Hii Ndio Njia Moja Muhimu Ya Kufikia Mafaniko Makubwa.
Kuondokana na tatizo hili, panga kufanya mambo ambayo ni muhimu kwako kitu cha kwanza kabisa asubuhi. Usitumie muda huu mzuri kufanya mambo yasiyokuwa na faida kwako. Kwa mfano mimi kila siku asubuhi kitu cha kwanza kabisa ninachofanya ni kuandika. Hii ni kazi inayohitaji kufikiri sana na kuwa na utulivu hivyo huwa naifanya nikiwa na utashi wa kutosha. Kwa mfano ninapoandika sentensi hii ni saa kumi na mbili na dakika 27 asubuhi na nimeanza kuandika kuanzia saa kumi na dakika 10 asubuhi. Hii ni makala ya tatu naandika. Kama ingekuwa ni jioni nisingeweza kuwa na kasi hii kubwa ya kuandika.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
TAMKO LA LEO;
Kuanzia sasa nitakuwa na matumizi mazuri sana ya utashi wangu. Kwa sababu najua utashi unapungua kadiri ninavyofanya mambo mengi, nitatenga muda wa asubuhi kuwa maalumu kwa mambo ambayo ni muhimu sana kwangu kufikia mafanikio makubwa.
Tukutane kwenye ukurasa wa 92 kesho.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment