Hakuna anayekataa kwamba elimu ni muhimu sana tena sana. Na elimu zote mbili yaani rasmi na isiyo rasmi ni muhimu sana ili kuweza kuyakabili mazingira yetu, kupambana na changamoto tunazokutana nazo na hata kuboresha maisha yetu. Elimu ni muhimu kwa ajili ya kufikia maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Lakini ELIMU SIO UFUNGUO WA MAISHA ila elimu inakuwezesha wewe kuweza kuutumia vizuri ufunguo wa maisha.
Ufunguo wa maisha ni ule uwezo mkubwa ambao upo ndani ya kila mtu, ni kile kipaji ambacho mtu anaweza kukitumia kufanya mambo makubwa sana na kwa bahati mbaya sana elimu haimpatii mtu kitu hiki na wakati mwingine inakiua kabisa.
Ingelikuwa elimu ni ufunguo wa maisha basi tungetegemea kila mtu aliyesoma awe na maisha bora sana tofauti na yule ambaye hajasoma. Lakini huu sio uhalisia, watu wengi wamesoma ila na wengi pia wana maisha magumu kuliko hata wale ambao hawajafikia kiwango kikubwa cha elimu.
Nasisitiza tena elimu ni muhimu sana lakini kama hujaujua ufunguo wa maisha yako ni nini elimu haiwezi kukupatia kitu hiko. Unahitaji kujua ni nini ambacho kipo ndani yako na ni jinsi gani unaweza kukiboresha kwa elimu ambayo utaipata. Kama utaendelea kuamini kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha utashindwa kugundua kile hasa kilichopo ndani yako na kufikiri kwa kupata elimu tu kila kitu kitakwenda vizuri.
Tunaishi kwenye dunia ambayo changamoto ni nyingi sana, kazi ni ngumu kupatikana na biashara zina changamoto nyingi kwa sababu kila mtu anaweza kufanya biashara zinazofanyika. Kitakachomfanya mtu aonekane sio tu elimu aliyonayo, maana sasa hivi karibu kila mtu ana elimu kubwa, bali ni kipi cha ziada ambacho mtu unacho na hapa ndio UFUNGUO WA MAISHA unapoingia.
Hivyo basi ni wakati wa kile mmoja wetu kujua ufunguo wa maisha yake ni nini na kutumia elimu aliyopata kuweza kuutumia vizuri ufunguo huo ili aweze kuboresha maisha yake na kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.
Coach Makirita Amani.
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
0 comments:
Post a Comment