Kwanza kabisa, hakikisha hujengi uadui na mtu, jaribu kuishi bila ya kujiingiza kwenye matatizo na watu. Ila kama watu ndio watalazimisha kujiingiza kwenye matatizo na wewe basi leo nakupa njia bora kabisa ya kuweza kulipa kisasi.
Labda kuna watu ambao wanakupinga sana kwa kile ambacho unafanya. Labda kuna watu ambao wanakuwekea vikwazo ili tu ushindwe. Labda kuna watu ambao wanakazana usiku na mchana ili kuhakikisha wewe hufikii kile unachotaka. Na kwa hakika kundi hili ni kubwa sana.
SOMA; NENO LA LEO; Kisasi Bora
Je ni njia gani ambayo unaweza kutumia ili kupambana na kundi lote hili? Je unawezaje kulipa kisasi kwa watu ambao wamekuwa wanakazana kukurudisha nyuma na hata wakati mwingine kukuumiza?
Kwanza kabisa, kulipa kisasi kwa kurudisha mapambano ni sawana kumwaga petroli kwenye moto. Utawapa kila sababu ya wao kuendelea kukufanyia mashambulizi makali.
Njia bora kwako ya kulipa kisasi kwa watu hawa ni kuishi vizuri, kuwa bora zaidi na zaidi. Mtu anayekufanyia kila kitu ili ushindwe ataumia sana pale ambapo ataona unaendelea kufanikiwa sana. Kadiri anakazana kukurudisha wewe ndio unazidi kumuacha, hili linaweza hata likamuua kabisa.
SOMA; Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.
Ishi vizuri, kuwa bora sana kwenye kile ambacho unafanya. Hii ndio njia bora kabisa ya kulipa kisasi kwa wale wanaokurudisha nyuma, na wanaweza hata kufa kabisa.
Kama kuna chupa yenye tindikali, ikimwagika kidogo bado nyingi inaendelea kuwa ndani ya chupa. Hivi ndivyo ilivyo kwa watu wabaya, wanakumwagia wewe ubaya wao kidogo, ila mwingi zaidi upo ndani yao. Usiogope, jua ubaya umewajaa wao kuliko hata wanaokuonesha wewe. Kazana kuwa bora zaidi na acha wenye tindikali iwamalize yenyewe.
TAMKO LA LEO;
Najua kabisa ya kwamba njia bora ya kulipa kisasi ni kuwa bora zaidi, kuishi maisha mazuri na kuwa na mafanikio makubwa. Najua kwa kuwa na mafanikio makubwa nazidi kuwachanganya wale wanaonirudisha nyuma na wanaweza kufa kabisa. Sina muda w akujibizana na wanaonirudisha nyuma, nina muda wa kuboresha kile ninachofanya na kuishi maisha yangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa 106 kesho.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment