Naweza kusema sasa hivi nimekuwa mlevi wa kitu kimoja, kusoma. Na sio kusoma tu, bali kusoma vitu vizuri ambavyo vinanifanya kuwa tofauti, kufikiri tofauti na hata kupata maarifa zaidi.
Naweza kusema kw akujivunia kwamba chochote ninachofanya sasa kinatokana na maarifa makubwa ninayoyapata kwa kusoma vitabu. Nasoma vitabu vingi na kwa sasa nasoma angalau vitabu viwili kwa wiki, wiki nyingine nasoma zaidi ya hapo ila nahakikisha kila wiki sishuko chini ya hapo.
Mwaka huu 2015 lengo langu ni kusoma vitabu visivyopungua 150, ukichanganya na vingine zaidi ya 200 nimesoma kwa miaka miwili iliyopita, maarifa yangu yataongezeka maradufu.
Leo siandiki haya kukuonesha kwamba nasoma sana ila nataka nikushirikishe faida kumi ninazozipata kwa kusoma, ukiacha kuongeza maarifa ambacho ndio kila mtu anafikiria.
SOMA; Mambo Yamebadilika, Hatari Sio Hatari Tena, Salama Ndio Hatari...
1. Burudani.
Kusoma ni burudani na ni burudani ambayo haina madhara yoyote kwenye mwili wako au maisha yako. Kuna baadhi ya vitabu unapovisoma unapata hisia nzuri za kiburudani na unaona uzuri na utamu wa maisha.
2. Kuhamasika.
Tunaishi kwenye dunia ambayo inakatisha tamaa sana. Kila jambo ambalo unajaribu kufanya kuna watu watakuambia haiwezekani au kuna watu watajaribu kukuwekea vikwazo. Unapokuwa unasoma vitabu unapata hamasa kubwa sana ya kufanya kile unachotaka kufanya. Unaposoma maisha ya wengine na kuona jinsi walivyopitia magumu, unapata moyo kwamba inawezekana.
SOMA; USHAURI ADIMU; Usijenge Nyumba Kwenye Uwanja Wa Kukodi.
3. Mshauri(mentor)
Ni muhimu sana kuwa na mshauri wako, ambaye anakuonesha wapi pa kupita ili uweze kupata kile unachotaka. Mara nyingi mshauri huyu inabidi awe ameshapitia unakopitia wewe. Katika mazingira yetu ya kitanzania ni vigumu sana kupata mtu wa aina hii, na hata ukimpata anaweza asipate muda mwingi wa kwenda na wewe sawa. Ila vitabu, vitabu ni mentor mzuri sana. Unaweza kusoma maisha ya watu ambao wamefanikiwa kwenye kile unachofanya na wakakupa mwongozo mzuri sana.
4. Kuwa bora zaidi.
Licha ya kuongeza tu maarifa, kusoma kuna kufanya unakowa bora zaidi katika kila eneo la maisha yako. Kabla sijajingea tabia ya kujisomea nilikuwa mtu wa kuhukumu, kukwazika, kuchukia, kubishana na mengine mengi. Lakini yote hayo nimeyaacha sasa, sina tena muda wa kuhukumu kwa sababu najua kila mtu ana matatizo yake, kila mtu anachagua maisha yake. Sikwaziki tena wala kukasirishwa na mtu kwa sababu najua anayetaka kukukasirisha anataka na wewe uwe na matatizo kama aliyonayo yeye, nishakuwa mjanja, sinunui tena matatizo ya watu. Na kilicho bora zaidi sibishani, zamani nilikuwa nikiwa na wazo langu na mtu akalipinga, nabishana nae mpaka nihakikishe amekubaliana nami, lakini sasa sibishani tena, kwa sababu nimejifunza kama wazo lako ni sahihi huna haja ya kulipigania, maana mwisho wa siku ukweli utashinda. Na kama wazo lako sio sahihi pia huna haja ya kubishana maana hakuna atakayekusikiliza au kujali.
5. Kuishi maisha tofauti tofauti.
Mtu anayesoma vitabu anaishi maisha zaidi ya 1000 kabla hajafa, mtu asiyesoma vitabu anaishi maisha mamoja tu mpaka anakufa. Sasa unafikiri ni yupi ambaye anakuwa na maisha mazuri kati ya hawa wawili? Kitabu kinaweza kukutoa hapa na kukupeleka kwenye mapiramidi ya misri, kikakupeleka marekani, kikakupeleka china na kadhalika.
SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.
6. Kuandika.
Moja ya faida kubwa ninazopata kwa kusoma vitabu ni kuandika. Ndio huwezi kuandika kama husomi, nazungumzia kitu ambacho kinaweza kuwasaidia wengine. Huwa naandika kila siku, zamani ilikuwa maneno 1000 ninapoamka asubuhi lakini sasa ni zaidi ya maneno 2000. Fikiria pale unapohitaji kuandika kila siku, jumatatu mpaka jumatatu, mwaka mzima, ni kazi ngumu eh? Kuna siku naweza kuamka sijisikii kabis akuandika, nachukua kitabu na kuanza kusoma, nusu saa baadae nakuwa nimepata mawazo zaidi ya matano ya kitu ninachotaka kuandika. Mara nyingi mawazo hayo hayatoki kwenye kitabu hiko ninachosoma, ila kile kitendo cha kukaa na kuanza kusoma ni kama milango ya akili inafunguka na kuanza kumwaga mawazo mazuri. Napenda sana hii hali.
7. Kutunza muda.
Unapoanz akujijengea tabia ya kujisomea, moja kwa moja unaanza kujijengea tabia ya kutunza muda. Hutapoteza tu muda na kuona huna cha kufanya kwa sababu muda wote una kitabu cha kusoma. Na pale ambapo una kitu cha kukusukuma umalize kitabu haraka kila dakika chache utakazopata utazitumia vizuri kusoma.
8. Kupunguza gharama.
Unapojijengea tabia ya kujisomea, muda wako mwingi unautumia kusoma hivyo hutapata mawazo ya nifanye nini sasa na kujikuta umeenda kufanya jambo ambalo linakuingiza kwenye gharama ambazo sio za msingi. Naweza kuhitaji kubadili mazingira nikachagua kwenda kwenye hoteli kubwa, nikiwa na kitabu nasoma, naagiza maji ya kunywa. Natulia na kusoma hata kwa masaa mawili bila ya kufanya kingine chochote. Ila ukiend akwenye hoteli ya aina hii na huna kitu cha muhimu cha kufanya, utajikuta unatumia gharama kubwa sana.
SOMA; Acha Kuifanya Hali Mbaya Kuwa Mbaya Zaidi.
9. Kuepuka umbea na majungu.
Angalau watanzania tumebobea kwa hili. Kama unapenda kufuatilia umbea na majungu sikulaumu kwa sababu kama huna kingine cha kufanya utafanya nini sasa? Yaani umeamka asubuhi huna ratiba yoyote ya siku zaidi ya kwenda kazini kama ulivyoenda jana. Utaanza kuangalia I nini kinaendelea, Diamond ana mpenzi gani mpya, kampa mimba nani, kavaa viatu vya shilingi ngapi au valentine alitumia kiasi gani cha fedha. Sawa, sikukatazi kufuatilia, ni burudani, lakini kabla ya kuipa burudani hii kipaumbele je maisha yako umeyapa kipaumbele?
10. Kuongeza kipato.
Hii ipo karibu sana na kupata maarifa maana maarifa ndio yanafanya kipato chako kuongezeka. Lakini nimetaka niiweke yenyewe ili kuonesha msisitizo zaidi. Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, nilisoma kitabu cha Robin Sharma, na moja ya vitu alivyoshauri ni hiki; KUONGEZA KIPATO CHAKO MARA MBILI, ONGEZA KUSOMA KWAKO MARA TATU. Nikasema nafanyia kazi hilo, kadiri ninavyojisomea ndivyo kipato changu kinaongezeka, mpaka wakati mwingine nashangaa nilichelewa wapi sikuanza mapema kama miaka kumi iliyopita.
Hizo ndio faida kumi za kujijengea tabia ya kujisomea. Anza kujisomea leo, na utaanza kunufaika na hayo na mengine mengi ambayo sijayaandika hapa. Nina uhakika na haya ninayokuambia hapa, hebu anza kufanya na lazima utaona mabadiliko.
SOMA; Habari Za Kusikitisha; Kila Kitu Kinabadilika…
KARIBU KWENYE KUNDI LA KUJISOMEA;
Kama unataka kujijengea tabia ya kujisomea na ungependa kupata kitu cha kukusukuma uweze kusoma nakukaribisha kwenye kundi la kusoma vitabu. Kundi hili linaitwa VORACIOUS READERS, katika kundi hili tunasoma vitabu viwili kwa wiki na ni muhimu kila mwanachama kusoma na kujadili angalau kitabu kimoja. Kupata maelezo zaidi ya kundi hili bonyeza maandishi haya.
MUHIMU; Usitake kujiunga na kundi hili kwa sababu tu umehamasika, ni muhimu sana utenge muda wa kujisomea na usome kweli, usipofanya hivyo unaondoka kwenye kundi.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA KUBORESHA MAISHA YAKO.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment