Sasa hivi tunaishi kwenye dunia ambayo vitu vimekuwa havina ukomo tena. Sasa hivi unaweza kuwa na mawasiliano masaa 24 kwa siku na siku 7 kwa wiki. Mitandao ya kijamii inakuonesha kila kitu na kwa muda wowote. Imetokea ajali mbali huko, ndani ya dakika chache unazopicha zote za ajali. Ni maendeleo au siyo? Kweli ni maendeleo ila kushindwa kuyatumia maendeleo haya vizuri kimekuwa chanzo cha matatizo kwa wengi.
SOMA; Kama Umeajiriwa Na Hujaanza Kufanya Hili Jua Kuwa Unapotea.
Maendeleo haya yametufanya tuone tunatakiwa kukamilisha kila kitu. Tofauti kati ya kazi na mapumziko haipo tena. Sasa hivi mtu anakuwa anafanya kazi muda wote na anapumzika muda wote. Mtu yupo katikati ya kazi, anaweza kuchungulia kidogo kwenye mitandao ya kijamii, kupata habari mbalimbali na akaendelea tena na kazi. Akiwa amepumzika ndio mwanzo mwisho kwenye mitandao. Hata mawasiliano ya kikazi sasa hivi yanamfikia mtu muda wowote hata kama ni usiku. Mtu anaweza kupata barua pepe ya kikazi hata kwenye muda ambao yuko mapumziko, na akalazimika kuijibu barua pepe hiyo.
Hali hii imesababisha watu tunachoka sana huku tukiwa na uzalishaji mdogo sana. Mitandao hasa ya kijamii inatupotezea muda mwingi na kutufanya tushindwe kufanya kazi iliyo bora.
SOMA; Kuwa Tone La Asali…
Cha kufanya; wakati wa kazi fanya kazi, mitandao ya kijamii achana nayo. wakati wa mapumziko, kuwa na muda maalumu utakaoweza kutembelea mitandao hii ili ujue ni nini kinaendelea. Baada ya hapo ondoka na upate muda wa kupumzika. Usishinde kwenye mitandao ya kijamii siku nzima, watu wenye mafanikio hawafanyi hivyo.
TAMKO LA LEO;
Najua ili niweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yangu, nahitaji kutumia muda wnagu vizuri. Nahitaji kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, nahitaji kuwa na muda wa kupumzika. Najua mitandao ya kijamii ni mwizi mkubwa wa muda wangu. Sitakubali mitandao hii iendelee kuiba muda wangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa 127 kesho.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365 bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment