Siku za hivi karibuni kumetokea machafuko nchini Afrika Kusini yaliyosababishwa na wananchi ambao ni wazawa wa nchi hiyo, kuwavamia na kuwafukuza wananchi ambao ni raia wa nchi nyingine. Machafuko hayo sio ya kwanza kutokea kwa Afrika Kusini na hata kwa Afrika kwa ujumla. Kumekuwepo na maandamano na machafuko ya aina hii tangu nchi hizi zimepata uhuru.
Leo nataka tujifunze kitu kutokana na machafuko ya aina hii na ni kitu gani tunaweza kufanya sisi Watanzania ili tusijikute kwenye hali kama hizo. Sitaangalia sana upande wa kisiasa kwa sababu lengo la andiko langu hili na kama yalivyo maandiko yangu mengine ni kuangalia hatua gani mimi na wewe tunachukua ili tusijikute kwenye hali ambazo hatuzipendi. Sio kulaumu wala kulalamika, bali kuchukua hatua.
Sababu halisi ya ubaguzi wa kiraia(xenophobia).
Kuna sababu nyingi sana ambazo zinaelezwa kusababisha machafuko ya aina hii. Lakini kuna sababu moja kubwa sana ambayo inabeba sababu nyingine zote. Sababu hiyo ni hali ngumu ya maisha na ukosefu wa ajira.
Kadiri siku zinavyozidi kwenda hali ya maisha inakuwa ngumu sana. Jamii inagawanyika kwenye makundi mawili, kundi moja dogo la wenye hali nzuri na kundi jingine kubwa ambalo linaendelea kukua kila siku la watu wenye maisha magumu sana. Hawa wenye maisha magumu mambo yao yanazidi kuwa magumu kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira ambalo linasumbua dunia nzima kwa sasa.
Katika hali kama hii wananchi wazawa, wenye hali ngumu na ambao mara nyingi wanaitegemea serikali itatue matatizo yao, wanaendelea kuweka matumaini yao kwa serikali. Lakini wananchi ambao sio wazawa, ambao wanajua serikali haipo kwa ajili yao wanaweka juhudi, wanafanya kazi za ajabu na hatimaye maisha yao yanakuwa bora kuliko ya wale wazawa. Sasa kadiri siku zinavyokwenda, hawa wageni wanaendelea kuweka juhudi na maisha yao yanakuwa bora, huku wazawa wakiendelea kuilalamikia serikali ifanye jambo.
SOMA; ONDOKA NYUMBANI
Unafika wakati sasa wazawa wanazidi kuwa na hali ngumu na wakiangalia wageni wana hali nzuri, hapa ndipo wanageuka na kuona kumbe adui yao ni mgeni. Kwa nini kwenye nchi yao wenyewe wawe na maisha magumu wakati kuna wageni ambao wanaishi kwa starehe. Hiki ni kitu ambacho kinawaumiza na kushinda kujizuia hivyo kuona suluhisho pekee ni kutumia wingi wao kuwaondoa hawa wageni.
Kwa akili za haraka wazawa watakubaliana wanachofanya ni sahihi, ila unapokuja kufikiri kwa kina unaona jinsi gani wazawa wanajipoteza na kumuacha adui halisi kwa kugombana na mtu ambaye sio hata adui.
Watanzania tunajifunza nini katika hili?
Yalipotokea machafuko haya Afrika Kusini, watanzania tulilipuka sana kulaani matendo yale. Kila mtu aliongea kwa uchungu ni jinsi gani kitendo walichofanya waafrika kusini kilikuwa cha kinyama. Ila baada ya hapo kila mtu aliendelea na mambo yake. Sina hakika sana kama kuna somo lolote ambalo tulijifunza kama taifa ili na sisi tusiingie kwenye hali kama ile. Na kwa kutojifunza chochote tunajiweka kwenye hatari kubwa ya kuja kurudia makosa ambayo wenzetu wameyafanya.
Kwa ufupi sana naomba nikushirikishe mambo ambayo watanzania tunapaswa kujifunza kwenye machafuko yaliyotokea Afrika Kusini.
1. Uzawa hautakubeba, juhudi ndio zitakubeba.
Kuna wakati ambapo tunafikiri kwamba sisi tunastahili zaidi kwa sababu ni wazawa. Ndio ni kweli, wewe wa nyumbani unastahili kupewa kipaumbele. Lakini kabla ya kupewa kipaumbele umeonesha nini. Hautabebwa kwa sababu wewe ni mzawa, utabebwa kwa sababu wewe unakitu muhimu kinachotakiwa. Tunaona makampuni mengi yanakwenda kuwekeza Lindi na Mtwara kwa sababu kuna gesi. Kampuni haitakupa wewe kazi kWa sababu tu ni mzawa, itakupa wewe kazi kwa sababu unazo sifa za kufanya kazi husika, Na hata kama kazi haihitaji sifa, basi unaonesha juhudi kwenye kazi unayopewa.
Hakuna kampuni inayopenda kuajiri raia wa kutoka nchi nyingine, kama ingeweza kupata wazawa wenye uwezo wa kufanya kazi husika. Ni gharama zaidi kuajiri raia wa nje kuliko raia wazawa.
Watanzania tujiandae sana kwa hili. Tumekuwa tunaona mambo machache ambayo sasa hivi bado hayajatuumiza ila kama hatutachukua hatua itakuwa tatizo baadae. Kwa mfano walimu wa shule nyingi za chekechea na msingi zinazoendeshwa kwa mchepuo wa wa kiingereza ni wakenya na waganda. Na wengi wao hata hawana taaluma ya ualimu, ila wanaweza kuongea kingereza kilichonyooka na cha kujiamini hata kama wanakosea. Sasa mchukue mhitimu wa chuo wa Tanzania mwambie aongee kingereza mfululizo kwa nusu saa kama hatakuwa bubu. Asilimia kubwa hawawezi hivyo, sasa mtu anayeteka kuwafundisha watoto kiingereza unataka akuajiri wewe kwa sababu tu ni mzawa na wakati huwezi kuongea kiingereza?
Hata tukija kwenye kazi ambazo hazihitaji elimu, bado watanzania sio watu wa kujituma na kuweka juhudi. Ukienda kwenye hoteli kubwa ukikuta wahudumu wa tanzania na wa nchi nyingine utaiona tofauti kabisa. Tunahitaji kuamka watanzania na tuanze kuweka juhudi na tujenge sifa zitakazotuwezesha kupewa upendeleo.
2. Dunia inakuwa kijiji, ondoka kwenye zama za mawe.
Ni jambo la kushangaza kama utafurahia kuvaa nguo iliyotengenezwa china, simu iliyotengenezwa china, mswaki uliotengenezwa kenya, chakula kilichoandaliwa ulaya na mengine mengi halafu ukahubiri uafrika kwanza, Utanzania kwanza. Haya mambo yanakufa, mawasiliano yamerahisisha sana biashara na muingiliano wa watu wa nchi mbalimbali. Hatuwezi kutumia nguvu kupinga hili, ila tunatakiwa kujiandaa na kuwa vizuri ili tuweze kupambana.
Kila siku Tanzania tunalaumiwa kukwamisha muungano wa Afrika Mashariki kwa sababu tunasema wananchi hawajawa tayari bado. Sasa sijui tutakuwa tayari lini. Na sisi wenyewe tunajitamba kwamba majirani wanatuonea wivu ndio maana wanakazana tuungane. Sawa, tunawakatalia wakenya na warwanda, huku wachina wakijazana kwenye nchi. Tunahitaji kuona kwamba dunia inakwenda haraka sana, hatuwezi kujifungia hapa tukifanya mambo yetu kwenye zama za mawe na kufikiri tutaweza kwenda na kasi ya dunia. Tutaachwa nyuma tu.
3. Tujue chanzo halisi cha matatizo yetu.
Kwa kutojua chanzo halisi cha matatizo yetu, umasikini wetu, utafika wakati tutaona kila tajiri ni adui yetu. Tutaanza kuwapiga matajiri na wakiisha tutageukiana wenyewe. Tatizo sio mchina aliyekuja hapa kufanya biashara, tatizo sio mkenya anayepata kazi wakati wewe hupati, tatizo linaanzia kwako.
SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.
4. Tusitegemee serikali ndio itatutoa hapa tulipo.
Ndio nakubali serikali ina nafasi yake ya kuweka sera bora kwenye nchi ambazo zitawawezesha wanachi kunufaika na rasilimali zinazowazunguka. Ila linabaki kuwa jukumu lako kuchangamkia fursa za kuweza kutumi rasilimali hizo. Katika utawala wa Mwl J K Nyerere waliona hawawezi kuyachimba madini kwa sababu hatukuwa na wataalamu wa kutosha. Ikapita miaka zaidi ya 30 na baadae ikaja sera ya uwekezaji. Migodi ikabinafsishwa kwa wageni, bado hatukuwa na wataalamu wa kutosha na hata leo hii miaka 54 baada ya uhuru bado hatuna wataalamu wa kutosha hasa kwenye sekta hii mpya ya gesi. Ndio unaweza kuilaumu serikali sana, lakini mwisho wa siku swali linarudi kwako, ni jitihada gani ambazo umefanya za kukuwezesha na wewe ukanufaika na rasilimali hizi. Ardhi sasa hivi inaonekana ipo na ya kutosha tu, hakuna anayeweka juhudi kubwa za kuitumia, kuna wajanja wameanza kuinunua kwa kasi, hakuna anayeona. Baada ya muda ardhi nyingi itakuwa mikononi mwa wachache na masikini watakuwa hawana hata kasehemu ka kulima mazao ya chakula, hapa ndio matatizo yatakapoanzia.
Naomba niishie hapa kwa leo, lakini tukubaliane ya kwamba sisi watanzania tunayo kazi kubwa ya kufanya ili tusijekuingia kwenye machafuko yatakayosababiswa na wachache kuwa na hali nzuri huku wengi wakiteseka. Sisi wananchi ndio tuna nguvu hiyo, tuhamasishane, tuelimishane na tuweke serikali ambayo itatuwezesha sisi kwa kutumia juhudi zetu kuwa sehemu ya neema ya nchi hii. Na sio kutegemea kupendelewa kwa sababu tu sisi ni wazawa.
Nakutakia kila la kheri mwananchi mwenzangu.
0 comments:
Post a Comment