#ONGEA_NA_KOCHA
Kwa miaka mingi dunia imekuwa inatupima kwa mambo haya mawili makuu...
Wanawake wamekuwa wakipimwa kwa kuonekano wao. Ni mzuri au sio mzuri?
Wanaume wamekuwa wakipimwa kwa umiliki wao. Je ana hela au hana hela, ana mali au hana mali?
Jamii nzima tumekuwa tukifanya hivi japo kwa unafiki tunaweza kukataa.
Vipimo hivi vimekuwa vinawazuia watu wengi kushindwa kufikia mafanikio kwa sababu tu wanatengwa na vipimo hivi.
Kama jamii inasema mwanamke mzuri ndio anaweza kuwa na maisha mazuri, kuna makabila mwanamke mweupe mahari yake ni kubwa kuliko mweusi, yule ambaye anakosa sifa hii atajiona hawezi kuwa na maisha mazuri.
Kama jamii inasema mwanaume mwenye hela ndio wa maana, kwenye jamii zetu wanaosikilizwa ni wenye hela hata kama hawana mawazo mazuri, ambaye anakosa sifa hii atajiona yeye sio wa maana na hivyo kujiondoa kabisa kwenye njia ya mafanikio.
Sasa mimi kama kocha wako nakutangazia rasmi kwamba achana kabisa na vipimo hivi vya hovyo.
Wewe ni zaidi ya vipimo hivi vilivyowekwa na jamii. Haijalishi una uzuri au ubaya, wewe ni bora sana. Haijalishi una fedha au huna fedha wewe ni mtu wa kipekee.
Endelea kuweka juhudi kwenye kile unachofanya na usikubali jamii ikuyumbishe na vipimo vyao visivyo na maana.
Wewe ni wewe, ni wa kipekee, ni bora na una mengi yaliyo mbele yako. Yaendee.
Makirita Amani,
www.amkamtanzania.com