Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Wednesday, December 31, 2014

Kozi 1100 Unazoweza Kujifunza Bure Kupitia Mtandao.

Mwaka 2015 ndio huu hapa, una nafasi kubwa ya kuanza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako kuanzia leo.
Ili uweze kubadili maisha yako, elimu ni muhimu sana.
Ni muhimu sana kujifunza na kuongeza maarifa ili kuweza kuwa na utaalamu utakaokufanya ufanye kazi nzuri na ya kipekee itakayokuwezesha kuboresha maisha yako.
Na dunia ya sasa imebadilika sana, kupata elimu sio lazima ukakae darasani siku nzima, ufundishwe na walimu ambao wanakuwa wanakutishia na mtihani na wakati mwingine usome vitu vingi ambavyo hata hutavitumia.
Dunia ya sasa imerahisishwa sana kiasi kwamba hapo ulipo unaweza kupata mafunzo makubwa sana yanayokuwezesha kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa.
Hapa nakupatia sehemu ambayo utaweza kujifunza chochote unachotaka bure kabisa. 
Unaweza kujifunza kuhusu kompyuta, mitindo, upishi, biashara, uchumi, uhasibu, historia, lugha, sheria, uandishi wa habari, dini, siasa, falsafa, hesabu, na chochote kile unachohitaji wewe ili kuboresha kazi au biashara zako.
Kitu kizuri zaidi kuhusu elimu hii ni kwamba unaweza kujifunza kwa njia ya video au audio yaani kuangalia au kusikiliza.
Nakushauri sana uchague japo kozi moja na uisome, nakuhakikishia hutakosa kitu cha kukufanya uwe bora zaidi.
Kuzipata kozi hizo BONYEZA MAANDISHI HAYA.

NENO LA LEO; Wazazi Wanavyojenga Au Kubomoa Maisha Ya Watoto Wao

It is not what you do for your children, but what you have taught them to do for themselves, that will make them successful human beings. –Ann Landers
Sio kile unachowafanyia wanao ndio muhimu, bali kile ulichowafundisha kufanya kwa ajili ya maisha yao ndio kitawafanya wafanikiwe.
Umekuwa ni utamaduni wa wazazi kutaka kuwafanyia watoto wao kila kitu ili wawe na maisha bora. Ila pale wazazi wanapoondoka watoto hawa wamekuwa wanapata shida sana.
Ni muhimu kuwafundisha watoto jinsi ya kutengeneza maisha yao wenyewe badala ya wewe mzazi kujaribu kuwajengea maisha, hutawasiadia kwa kuwajengea maisha yao.
Nakutakia siku njema.

Tuesday, December 30, 2014

Kesho Jua Litachomoza Tena...

Kesho asubuhi jua litachomoza tena, kama lilivyochomiza leo, jana na siku zote zilizopita.
 Hii ina maana kwamba haijalishi leo mambo yako yamekwenda vibaya kiasi gani, kesho ni siku mpya na unaweza kubadili maisha yako.
 Kesho jua litachomoza tena hata kama kutakuwa ja mawingu.
 Hii ina maana kwamba hata kama unapitia matatizo mengi kiasi gani, usikubali yakufanye upoteze muelekeo.
 Jifunze kutokana na changamoto unazopitia huku ukifurahia maisha yako.

Matatizo Yote Kwenye Maisha Yako Yanatokana Na Kitu Hiki.

Kila mmoja wetu anapitia matatizo au changamoto mbalimbali kwenye maisha yake. Inawezekana unapitia matatizo ya kuumwa, au mwingine anapitia changamoto ya madeni na pia inawezekana unapitia changamoto ya migogoro kwenye familia.
Sasa matatizo yote haya huwa yanaanza na kitu kimoja.
Kabla sijakuambia kitu hiko naomba nikuoe mfano mmoja mzuri sana.
Ukitaka kumuua chura kwa maji ya moto huwezi kumuua kwa kumweka kwenye maji ya moto. Chura ni mnyama ambaye anavyopata joto kali anakuwa na nguvu ya kuweza kuchukua hatua haraka. Hivyo ukimweka kwenye maji ya moto ataruka haraka sana kuondoka kwenye maji hayo.
Sasa hapa kuna njia rahisi ya kumuua chura kwa maji ya moto. Unachukua maji ya baridi kabisa, tena yenye barafu halafu unamweka chura. Kwenye baridi chura hana nguvu ya kuondoka. Baada ya hapo unaanza kupasha maji yale taratibu, kadiri maji yanapata joto chura anakuwa anafurahia, anaona utamu. Akija kustuka maji yanakaribia kuchemka na mwili mzima umesaishiwa nguvu.
Hivi ndivyo matatizo uliyonayo yalivyoanza;
Hukujikuta siku moja unaumwa tu, bali zilianza dalili ndogo ndogo ukazipuuzia.
Hukujikuta kwenye madeni tu, bali ulianza uzembe mdogo mdogo kwenye fedha na ukapuuzia,
Hukujikuta kwenye mgogoro mkubwa wa kifamilia kwa mara moja tu, bali vilianza vitu vidogo vidogo ukavipuuzia.
Hatimaye mambo yamekuwa mambo na sasa upo katikati ya matatizo.
Kupuuzia dalili ndogo ndogo ambazo zingeweza kushughulikiwa ndio kunakufikisha kwenye matatizo makubwa.
Kama waswahili wanavyosema; usipoziba ufa....

Mambo Kumi Muhimu Kuhusu Maisha

1.Tupo hapa kujifunza, dunia ndio mwalimu wetu.

2. Ulimwengu hauna upendeleo.

3. Maisha yako ni matokeo ya imani yako.

4. Pale utakapoanza kutegemea zaidi vitu, watu au fedha unaharibu kila kitu.

5. Kila unachokiwekea mkazo kwenye maisha yako kinakua.

6. Fuata moyo wako.

7. Mungu hatoshuka kutoka mawinguni na kukuambia “sasa hivi una ruhusa ya kufanikiwa”

8. Unapopigana na maisha maisha siku zote yanashinda.

9. Unawapendaje watu? Kwa kuwakubali.

10. Mpango wetu hapa duniani sio kuibadili dunia bali kujibadili sisi wenyewe.

Kama Hutofanya Chochote…

Kama hutofanya chochote hakuna kitakachotokea…

Kama ukifanya chochote, chochote kinaweza kutokea…

Ndio unaweza kuishia huna kitu, lakini hapo ndio ulipoanzia.

Una nini cha kupoteza?

Fanya kitu kubadili maisha yako sasa.

NENO LA LEO; Njia Isiyokuwa Na Foleni.

There are no traffic jams along the extra mile. –Roger Staubach

Hakuna foleni unapokwenda mbali zaidi.

Unapofanya kile ambacho kila mtu anafanya utakutana na ushindani mkubwa sana.

Unapofanya kitu chenye ubora mkubwa na wa kipekee utakuwa mwenyewe na hakutakuwa na ushindani.

Mara zote nenda maili ya ziada, fanya zaidi ya wengine na utapata zaidi.

Nakutakia siku njema.

Monday, December 29, 2014

Kitu Hiki Kimoja Kitakufanya Uweze Kujiajiri, Uishie Kuwa Mwajiriwa Au Uishie Jela.

Habari za jumatatu rafiki?
Tunaelekea kabisa ukingoni mwa mwaka 2014.
Najua unefanikiwa mengi, umepata changamoto kwenye machache na umejifujza mengi pia.
Najua pia unajiandaa vyema kwa mwaka 2015
Leo nataka tukumbusane kitu muhimu sana ambacho ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuzingatia.
Kitu hiko ni NIDHAMU...
Unapoweza kuwa na nidhamu ya kujisimamia wewe mwenyewe yaani jidhamu binafsi unaweza kujiajiri, kuwa mjasiriamali au kufanya biashara.
Unaposhindwa kuwa na nidhamu ya kujisimamia mwenyewe utahitaji mtu wa kukusimamia na hivyo utapata mtu wa kukuajiri na utakuwa muajiriwa, ukijaribu biashara itakushinda.
Unapokosa Nidhamu kabisa, yaani huna nidhamu kabisa unaishia kukaa jela.
Fanya maamuzi mazuri mwaka 2015, jijengee nidhamu binafsi.
Kama hujui uanzie wapi ili kujijengea nidhamu binafsi jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, tumejadili hatua kwa hatua jinsi ya kujijengea tabia hii.
Tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz na ujiunge.
Nakutakia kila la kheri.
TUPO PAMOJA.

Hiki Ndio Kitakachotokea Miaka 100 Ijayo..

Sio kwamba nimekuwa mtabiri ila nina uhakika miaka mia moja ijayo kitu hiki kitatokea.
Kitu hiko ni kwamba wote tunaosoma hapa tutakuwa tumekufa. Ndio namaanisha hata wewe utakuwa umekufa miaka mia moja ijayo kuanzia leo, yaani mwaka 2114.
Na kwa bahati nzuri sana tutakuwa tumekufa kwa kipindi kirefu sana, kwa miaka zaidi ya trilioni inayokuja tutakuwa tumekufa.
Nakwambia yote haya ili nini, si unayajua?
Nataka ufanye nambo mawili;
1. Ishi maisha yako kwa furaha maana muda unaoishi ni mfupi kuliko ambao utakuwa umekufa.
2. Hakikisha unagusa maisha ya wengine ili utakapoondoka uache kumbukumbu ya kuwepo kwako. Kujua jinsi ya kufanya hivyo soma makala hii; sio wote tunaowazika wamekufa.
Kila la kheri.

NENO LA LEO; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kufanikiwa.

In order to succeed, your desire for success should be greater than your fear of failure. –Bill Cosby

Ili kufanikiwa, hamu yako ya mafanikio inabidi iwe kubwa kuliko hofu yako ya kushindwa.

Kinachokufanya mpaka sasa hujafanikiwa ni hofu ya kushindwa. Una hofu kwamba ukijaribu kitu fulani unachokifikiria utashindwa.

Ili ufanikiwe inabidi uweze kuishinda hofu hiyo na utaweza kuishinda kama kiu yako ya kufanikiwa ni kubwa kuliko hofu ulizo nazo.

Nakutakia siku njema.

Sunday, December 28, 2014

NENO LA LEO; Hapa Ndio Pa Kuanzia, Hasa kwa mwaka 2015…

The way to get started is to quit talking and begin doing. –Walt Disney

Njia ya wewe kuanza ni kuacha kuongea na kuanza kufanya.

Ni rahisi sana kuongea, kila mtu anaweza kuongea..

Ni rahisi sana kupanga, kila mtu anapenda kupanga na kupanga tena baada ya kupanga.

Lakini kuongea na kupanga hakutofanya lolote, hakutokufikisha popote.

Kufanya ndio kutakutoa hapo ulipo, vitendo na sio maneno au mipango.

Acha kupanga na kuongea kila siku, 2015, maneno kidogo vitendo vingi..

Nakutakia siku njema.

Hiki Ndicho Kinachonisukuma…

Imani yangu.
Hiki ndicho ninachokiamini mimi na kinachonisukuma kila siku kufanya kile ambacho ninafanya;
Naamini kila mtu ana uwezo mkubwa ndani yake wa kuweza kuwa bora zaidi ya alivyo sasa.
Naamini kuna fursa nyingi sana zinazomzunguka kila mtu pale alipo ambazo zinaweza kumsaidia kuboresha maisha yake zaidi.
Nafanya kazi na watu kuwawezesha kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao na fursa zinazowazunguka ili kuweza kuboresha maisha yao na kufikia mafanikio makubwa.
Hiki ndio ninachokiamini, hii ndio itakuwa sala yangu kila siku kwa mwaka 2015.
Nataka wale ambao wanahitaji mabadiliko kweli kwenye maisha yao wakaribie kwenye KISIMA CHA MAARIFA ili tufanye kazi pamoja.
Tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz na ujiunge kisha nitumie meail kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz ili tuanze mpango kazi.

Sunday, December 21, 2014

Ishi na Waache wengine nao waishi...

Ishi na waache wengine nao waishi,
Fanya biashara na waache wengine nao wafanye biashara,
Vua samaki na waache wengine nao wavue samaki,
Kula raha na waache wengine nao wale raha...
Kuna fursa nyingi sana hapa duniani hivyo hakuna haja ya kiwabania wengine.
Kama ilivyo kwamba huweza kulinda bahari na kusema ni yako, ndivyo ilivyo kwa fursa.
Nakutakia kila la kheri.

Saturday, December 20, 2014

Hawa Ndio Watu Unaoishia Kuwa Nao...

Unaishia kuwa na watu ambao unawavumilia...
Marafiki ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye tabia ambazo unazivumilia na hakuna aliyekulazimisha uwe nao.
Wafanyakazi ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye ufanisi ambao unauvumilia na hakuna aliyekulazimisha kuendelea kuwa nao.
Wateja ulionao ni wale ambao unawavumilia, wenye tabia ambazo unazivumilia na hakuna aliyekulazimisha kuendelea kuwa nao.
Mwajiri uliyenaye ni yule unayemvumilia, mwenye tabia unazozivumilia na anayekupa kipato unachokivumilia, hakuna aliyekulazimisha uendelee kuwa naye...
Yote hii ina maana gani?
Maana kubwa ni kwamba MAISHA NI UCHAGUZI, unachagua nani awe rafiki yako, nani awe mwajiri wako, nani awe mfanyakazi wako na nani awe mteja wako.
Kama kuna ambaye unaona hafai kuwa mmoja kati ya hao, unamfukuza, unaachana nae na kujumuika na yule unayeendana nae.
Maisha yako, uchaguzi wako.

Adui Yako Anaanzia Hapo Ulipo Na Anaanza hivi.

Adui yako ni wewe mwenyewe na anaanza na hofu zako...
Una hofu ngapi leo asubuhi?
Una hofu kama utakula leo mchana na jioni?
Una hofu kama mshahara utaingia kabla ya krismas?
Una hofu kama krismasi yako itakuwa nzuri?
Una hofu kama baraza la mawaziri litabadilishwa au halitabadilishwa?
Una hofu kama serikali itafanya maisha kuwa rahisi zaidi?
Una hofu kama 2015 chama unachokipenda kitashika madaraka?
Una hofu kama mpenzi/mwenza wako atakusaliti/atakuacha?
Una hofu kama hofu zako zitaosha??
Karibu hofu zote hapo juu hazina msaada mkubwa kwako au huwezi kuziathiri. Na kuendelea kuziendekeza ndio zinakuzuia ushindwe kufikiria mambo makubwa yatakayokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
Yaani kichwa kimoja chenye hofu zote hizo kitapata wapi nafasi ya kuweka jambo la muhimu?
Hofu hizi ndio adui mkubwa wa mafanikio kwako...
Usizipeleke hofu hizi 2015....

Friday, December 19, 2014

Hiki Ni Kitu Unachotakiwa Kufanya Kila Siku...

Linapokuja swala la kuhamasika/kuhamasishwa sio kitu kinachotokea mara moja halafu ghafla unakuwa mtu uliyehamasika.
Hiki ni kitu ambacho kinatakiwa kutokea kila siku ya maisha yako.
Usifikiri unasoma kitabu kimoja unapata maarifa yote unayohitaji, unatakiwa kujifunza kila siku kila siku, yaani namaanisha KILA SIKU, kama jinsi ambavyo UNAOGA KILA SIKU na kama ambavyo UNAKULA KILA SIKU.
Ndio maana mambo haya sio rahisi, yanahitaji kujitoa, yanahitaji kujikana?
Je upo tayari?
Upo tayari kufanya mabadiliko kwenye maisha yako mwaka 2015?
Kama upo tayari niambie NDIO kwenye maoni hapo chini, halafu tuma email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz ukisema upo tayari halafu nitakupa mpango mzima.
Pia tembelea www.amkaconsultants.blogspot.com ili kujifunza kitu kipya kila siku.
Karibu sana, TUPO PAMOJA.

Wewe Ni Wa Kwanza Kusoma Hapa…

Ndio wewe ni wa kwanza kusoma hapa, yaani ndio unapata habari hii kwa mara ya kwanza na unaipata hapa tu.

Wewe ni wa kwanza kusikiliza wimbo huu mpya, na unausikia kwa mara ya kwanza kwenye kituo hiki cha redio tu.

Wewe ni wa kwanza kupata habari hizi mbaya za ajali, umezisikia hapa tu…

Kuwa wa kwanza kupata kila habari inayotokea, kila linalofanyika, masaa 24 kwa siku, siku saba bkwa wiki.

Swali; je ukishakuwa wa kwanza inabadilisha nini?

Kupenda kuwa wa kwanza kwa vitu ambavyo havina msaada mkubwa kwentu kunatufanya tushindwe kufuatilia yale ambayo ni ya muhimu kwetu.

Kwa mfano unasoma kwenye mtandao; mtu fulani maarufu amekufa, na wewe kwa kuwa unataka kuwa wa kwanza kutoa habari, unakimbilia kusambaza, bila hata ya kudhibitisha kweli kama amekufa.

NENO LA LEO; Hiki Ndio Unachokiishi

Too many of us are not living our dreams because we are living our fears. –Les Brown

Wengi wetu hatuishi ndoto zetu kwa sababu tunaishi hofu zetu.

Acha sasa kuzuiwa na hofu na anza kuishi maisha ya ndoto zako. Hakuna kinachoshindikana kama kweli utakuwa umedhamiria.

Nakutakia siku njema.

Thursday, December 18, 2014

NENO LA LEO; Huwezi Kuanguka Kama Hutafanya Hivi.

You can’t fall if you don’t climb. But there’s no joy in living your whole life on the ground. –Unknown

Huwezi kuanguka kama hutopanda. Lakini hakuna furaha kwenye maisha kama utaishi maisha yako yote ukiwa chini.

Anza sasa kupanda na kuwa bora zaidi, ndio unaweza kuanguka ila utajifunza mengi na utaweza kufikia juu zaidi.

Ukiendelea kuogopa kuanguka, utaendelea kubaki hapo ulipo.

Nakutakia siku njema.

Wednesday, December 17, 2014

Mabadiliko Yanaanzia Hapa...

Mabadiliko yanaanza na yule anayetaka mabadiliko...
Kama unataka watu wakuheshimu anza wewe kuwaheshimu...
Kama unataka watu wakupende anza wewe kuwapenda...
Kama unataka watu wafanye unachotaka anza wewe kufanya kitu hiko.
Ni vigumu sana kumlazimisha mtu afanye kile unachomtaka afanye.
Ila ni rahisi sana mtu kuiga kile unachofanya.
Badala ya kupoteza nguvu nyingi kumwambia mtu kwa nini abadilike, kwa nini usoelekeze nguvu hizo katika kuanzisha mabadiliko yenyewe?

Hili Ndilo Kaburi Unalozika Ndoto Zako Kubwa.

Jana ulipanga leo utaanza kuweka mipango ya kuanza biashara,
Au ulipanga leo utaanza mazoezi,
Au ulipanga leo utaanza kuweka akiba ya kila unachopata,
Au ulipanga utaboresha kazi yako zaidi...
Leo imefika, unajikumbusha kwamba unahitaji kufanya ulichopanga jana, lakini mwili haupo tayari kabisa kufanya.
Nafsi inaanza kukusuta, ulipanga leo utafanya, mbona hufanyi? Kwa haraka linakuja wazo linalotuliza nafsi yako.... NITAFANYA KESHO....
Baada ya wazo hili unaacha kujisuta na kukubali kwamba kesho mambho yataanza rasmi.
Na kweli kesho mambo yanaanza rasmi kweli, ila ni mambo kama uliyofanya leo, kusema utaanza kesho.
NITAANZA KESHO ni kaburi la ndoto kubwa sana. Ndoto nzuri na za kuboresha maisha yako umezizika kwenye kaburi hilo.
Acha sasa kuzika ndoto zako, kama kuna kitu muhimu unataka kufanya kwenye maisha yako, kifanye sasa, sio kesho.

Sunday, December 14, 2014

Nenda Kapige Kura, Au Usipige Na Fanya Hivi…

Leo ni siku ya kupiga kura kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa, najua unajua hili, ila imebidi niliandike tena ili tupate pa kuanzia. Kama ulikuwa hujui leo ndio siku ya uchaguzi basi tuna tatizo kubwa zaidi.

Kwa takwimu mbalimbali za chaguzi zilizopita tunaona idadi kubwa ya watu waliojiandikisha hawapigi kura. Na laiti kama watu hao wangepiga kura mabadiliko yangekuwa makubwa sana.

kupiga kura

Sasa sitaki kuandika mengi nikucheleweshe kupiga kura, ninachokuambia leo ni;

Nenda kapige kura, au usiende kupiga na usilalamike chochote.

Maana watanzania tumekuwa mafundi wa kulalamika ila hatua hatuchukui. Kama hatua kubwa za kuwawajibisha watu hatuwezi kuchukua, basi tuchukue hatua ya kupiga kura na kuchagua viongozi ambao ni bora.

Wahi kapige kura yako asubuhi hii, na mhamasishe kila unayekutana naye nae akapige kura.

Hapa ndipo mabadiliko ya nchi yetu yanapoanzia.

Saturday, December 13, 2014

Vitu Vitamu Muhimu Unavyohitaji Ili Kuingia Kwenye Biashara.

Ili kuingia kwenye biashara zama hizi unahitaji vitu vitatu tu;
i. Kidadavuzi mpakato(laptop)
ii. Simu ya mkononi yenye uwezo mkubwa(smartphone)
iii. Wazo.
Na wazo sio lazima liwe kubwa sana, linaweza kuwa wazo la kawaida sana ambalo wengine wanalipuuza.
Kama una vitu hivyo vitatu na hujui uanzie wapi niandikie kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Angalizo; uwe tayari kufanya kazi, sio lelemama...

Friday, December 12, 2014

NENO LA LEO; Hiki Ndio Chanzo Cha Furaha.

Happiness is not something readymade. It comes from your own actions. –Dalai Lama

Furaha sio kitu ambacho kimetengenezwa tayari. Furaha inatokana na matendo yako mwenyewe.

Kama utakuwa na matendo yenye maana kwako na kwa wanaokuzunguka ni lazima yatakuletea furaha. Furaha hupewi na mtu mwingine.

Soma; HII NI HAKI YAKO YA KUZALIWA, USITEGEMEE KUPEWA NA WENGINE.

Nakutakia siku njema.

Msitu Msituni…

Ukiwa mbali na msitu, yaani kabla hujaingia msituni utauona msitu ni mkubwa sana. Utaona eneo lote la msitu limejaa miti na huwezi kuona hata ardhi. Kwa umbali uliopo unaweza kuamini kwamba hakuna hata sehemu ya kupita kwenye msitu huo.

Ila unapoingia kwenye msitu huo, huoni tena msitu. Yaani unapokuwa msituni huoni tena msitu, bali unaona mti mmoja mmoja na kuna sehemu kubwa ya kupita. Unaweza kuupita mti mmoja baada ya mwingine na kuendelea kufanya yako…

Kabla hujaingia kufanya jambo lolote utaona vikwazo vingi sana, utaona hatari na ilivyo rahisi kushindwa. Ila unapoingia kwenye jambo hilo, vikwazo vilivyokuwa vinakutisha mwanzo unakuta sio vikubwa kama ulivyokuwa unafikiri. Unakuta ni changamoto ndogo ndogo ambazo unaweza kuzimudu.

Usiogope tena kufanya kile unachotaka kufanya, huwezi kuona msitu ukiwa msituni…

Nakutakia kila la kheri.

Wednesday, December 10, 2014

NENO LA LEO; Mlango Mpya Wa Furaha

When one door of happiness closes, another opens, but often we look so long at the closed door that we do not see the one that has been opened for us. –Helen Keller

Mlango mmoja wa furaha unapojifunza, mlango mwingine unafunguka, lakini tunaishia kuangalia mlango uliojifunza kwa muda mrefu na hivyo kushindwa kuona mlango mpya uliofunguka.

Acha kuangalia matatizo yako tuu, angalia pembeni na utaona fursa nyingi za kubadili na kuboresha maisha yako.

Nakutakia siku njema.

Waliofika kileleni…

Watu waliofika kwenye kilele kikubwa sio kwa sababu watu hao waliruka na kujikuta kileleni, ila kwa sababu watu hao, wakati wenzao wamepumzika wao waliendelea kukomaa na kuendelea na safari.

Endelea na safari yako wakati wengine wamelala…

Endelea na safari yako wakati wengine wanastareheka…

Endelea na safari yako wakati wengine wanabishana mambo ambayo hawawezi kuyaathiri…

Watakuona upo kileleni, wakati wao wakiendelea kusota na kushindwa kufika kwenye kilele.

Tuesday, December 9, 2014

Ana Miaka 53 Ila Bado Analishwa Uji…

Kwa kawaida mtu yeyote anayezaliwa huwa anapitia vipindi tofauti kwenye maisha yake.

Kwanza kabisa anaanza kama mtoto ng’aa, ambapo anakuwa anategemea kunyonya maziwa ya mama tu.

Anaendelea kukua na baadae anakuwa analishwa uji, huku akikazana kutambaa na hatimaye kutembea.

Baada ya muda anaanza kula matonge ya ugali na kukimbia mwenyewe..

Baadae kabisa anakuwa mtu mzima anayejitegemea na kuweza pia kuwasaidia wengine.

Mpaka kufika miaka 53, mtu anatakiwa awe ameshapitia vipindi vingi vya ukuaji na maendeleo kwa ujumla. Na huu ndio umri ambao anakuwa ameshakamilisha mambo mengi kwenye maisha yake na anaishi maisha ya furaha.

tz1

Sasa maajabu makubwa ni pale unapomkuta mtu mwenye miaka 53 bado analishwa uji. Yaani yeye tokea atoke kwenye hatua ya kwanza ya kunyonya amekwamba kwenye hatua ya pili ya kunyweshwa uji.

Kama akitishiwa kunyimwa uji huo anaolishwa anaanza kulia sana na kuona maisha yake yatakuwa magumu.

Sio kwamba mtu huyu alizaliwa na ulemavu wa aina yoyote, na wala sio kwamba amekosa nguvu au mbinu nyingine za kujitegemea, yeye amefurahia kulishwa uji na hataki kufikiria zaidi ya hapo.

Ni jambo la kushangaza sana unapomkuta mtu mzima, miaka 53, mwenye afya na nguvu akiendelea kulishwa uji…

NENO LA LEO; Ni Mara Ngapi Unahitaji Kusimama Tena?

Fall seven times and stand up eight. –Japanese Proverb

Anguka mara saba, nyanyuka mara ya nane.

Haijalishi ni mara ngapi umeshindwa, cha msingi ni kuendelea tena.

Kukata tamaa ni mwiko kama kweli unataka kuyafikia mafanikio makubwa.

Nakutakia siku njema.

Monday, December 8, 2014

NENO LA LEO; Jambo Kubwa Na La Kushangaza.

We can easily forgive a child who is afraid of the dark; the real tragedy of life is when men are afraid of the light. –Plato

Tunaweza kumsamehe mtoto mdogo anayeogopa giza; ila jambo kubwa na la kushangaza kwenye maisha ni pale mtu mzima anapoogopa mwanga.

Ni kipi unachokiogopa kukifanya kwenye mwanga? Maana hiko ndio kinachokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia siku njema.

Nyasi Za Upande Wa Pili Ni Za Kijani Zaidi…

Angalia zile nyasi za upande wa pili, ni za kijani zaidi ya nyasi zilizopo upande wako…

Hii ni fikra ambayo huwa inamjia kila mtu katika sehemu aliyopo iwe ni maisha, kazi au biashara.

Unaweza kuona wenzako wana maisha mazuri kuliko hayo uliyoko nayo kwa sababu tu unaona wanatembelea magari mazuri au wanaonekana sehemu nzuri nzuri…

Unaweza kuona kazi au biashara wanazofanya wengine ni nzuri na zinawalipa zaidi kuliko kazi au biashara unayofanya wewe…

nyasi

Hii sio kweli kabisa, unaziona nyasi hizo ni za kijani zaidi ya za upande wako kwa sababu hujafika kwenye nyasi hizo. Utakapo pata nafasi ya kufika kwenye nyasi hizo utagundua kwamba hazina tofauti kubwa na nyasi zako.

Thamini kile ulicho nacho na kama unataka kiwe bora zaidi, kiboreshe. Usiyumbishwe kwa kutamani wanayofanya wengine, huenda hata wao wanatamani unayofanya wewe.

Hivyo njia bora sio kuangalia nyasi zipi ni za kijani zaidi, bali zifanye nyasi zako kuwa za kijani zaidi.

Nakutakia kila la kheri.

Sunday, December 7, 2014

Tulikuona Wakati Unakuja Mjini…

Tulikuona wakati unakuja mjini, usijione mjanja leo…

Ulikuja umevaa yeboyebo na nguo umebeba kwenye mfuko wa rambo, leo unajiona unajua sana…

Hayo ni maneno ya hovyo sana yanayotolewa na watu walioshindwa. Watu ambao wamepoteza muda wao kwa kufikiri wao ni wakongwe na anakuja mtu na kuwaacha wakishangaa.

Ili kujifariji kwamba na wao wana kitu fulani wanatumia sababu hiyo ya ukongwe.

joti-mpoki-enzi-hizo

Sikiliza mafanikio hayapimwi kwamba ulizaliwa wapi au umekulia wapi. Mafanikio yanapimwa na nini unachoweza kuonesha watu kwamba umefanya na kimeleta mabadiliko kwenye maisha ya wengine.

Kama wewe ndio unaambiwa wakuja usihofu, endelea kukazana.

Kama wewe ndio unawaambia wenzako ni wakuja soma hapa; ONDOKA NYUMBANI. Itakusaidia sana na utajua ni hatua gani ya kuchukua.

Chukua hatua sasa…

NENO LA LEO; Hapa Ndio Unapoweza Kuanzia Na Hiki Ndio Unachoweza Kufanya.

Start where you are. Use what you have. Do what you can. –Arthur Ashe

Anzia hapo ulipo. Tumia hiko ulicho nacho. Fanya unachoweza.

Usipoteze tena muda kufikiri ni wapi pa kuanzia, uanze na nini au ufanye nini. Unachohitaji ni kuanza kupiga hatua na mambo mengine yote yatakwenda vizuri.

Nakutakia siku njema.

Saturday, December 6, 2014

Maswali matatu muhimu ya kujiuliza leo ili kujua muelekeo wa maisha yako.

Maswali matatu muhimu ya kujiuliza ili kujua ni nini unapaswa kufanya.
i. Ni kitu gani ambacho unajua unataka ukifanye ila bado unakipuuzia kukifanya?
ii. Ni kitu gani unaweza kukisimamia leo?
iii. Ni kitu gani haupo tayari kukiacha/kukiharibu hata kama kungetokea nini?
Kwa kujibu maswali haya utajua ni kipi muhimu kwako na anza kukifanyia kazi.
Kama bado unapata shida ya kujua ni kipi muhimu kwako karibu kwenye ushauri utakaokuwezesha kujijua zaidi. Andika email kwenda ushauri@kisimachamaarifa.co.tz
Nakutakia kila la kheri.

Bado Hujachelewa...

Kuna bwana mmoja alikuwa analalamika ni jinsi gani alikuwa anapenda kujifunza kupiga kinanda ila akakosa muda kwenye maisha yake.
"Kwa nini usianze sasa" rafiki yake alimuuliza.
"Unashangaza wewe" yule bwana alimjibu. "Nina miaka hamsini sasa, nikianza kujifunza leo itanichukua miaka mitano mpaka nijue kupiga kinanda vizuri, wakati huo nitakuwa na miaka hamsini na tano" aliongeza bwana yule.
Rafiki yake alimsikiliza kwa makini kisha akamuuliza, " kama usipoanza kujifunza kinanda leo, miaka mitano ijayo utakuwa na miaka mingapi"?
Katika simulizi hii fupi unaweza kuona ni jinsi gani tunajijengea vikwazo visivyo na msingi sisi wenyewe.
Kama kuna jambo lolote unalotaka kufanya kwenye maisha yako bado hujachelewa kulifanya, ANZA SASA...
Nakutakia kila la kheri,
Kama unahitaji ushauri wa kina juu ya jambo lolote linalokusumbua andika email kwenda ushauri@kisimachamaarifa.co.tz
Karibu sana.

Tunarudia Makosa Yale Yale…

Hakuna makosa mapya, tunarudia makosa yale yale.

Ila kwa kuwa teknolojia imekua basi na kiwango chetu cha kufanya makosa yale yale tuliyokuwa tunayafanya zamani kimebadilika.

Watu wamekuwa wakiambiwa wasiue zaidi ya miaka 4000 iliyopita sasa, lakini mpaka leo bado wanaua.

Usiibe, usizini, bado kila siku tunarudia makosa haya haya.

Hii ni kwa sababu sisi ni binadamu, na tunakosea kila mara. Lakini hii haituzuii kuwa bora zaidi ya tulivyo sasa. Tunaweza, tufanye.

NENO LA LEO; Chochote Unachotaka Kuwa Kipo Huku

Everything you’ve ever wanted is on the other side of fear. –George Addair

Chochote ambacho umewahi kutaka kipo upande wa pili wa hofu.

Acha sasa kuwa na hofu na chukua hatua kupata kile unachotaka.

Kumbuka hakuna kingine zaidi ya kuchukua hatua.

Nakutakia siku njema.

Friday, December 5, 2014

NENO LA LEO; Umepangiwa Kuwa Mtu huyu…

The only person you are destined to become is the person you decide to be. –Ralph Waldo Emerson

Mtu pekee uliyepangiwa kuwa ni yule unayeamua kuwa.

Kama unaamua kuwa na mafanikio utakuwa nayo kweli na kama unaamua kuwa wa hovyo utakuwa wa hovyo.

Maamuzi ni yako, uchaguzi ni wako.

Nakutakia siku njema.

Mwalimu Anakusubiri, Chukua Hatua Sasa…

Mwanafunzi anapokuwa tayari mwalimu hutokea…

Huu ni usemi wa kale kidogo ila unaobeba maana kubwa sana.

Mwanafunzi anapokuwa tayari mwalimu hutokea, sio kwa sababu mwalimu alikuwa anasubiri mwanafunzi awe tayari ndio ajitokeze bali mwalimu alikuwepo muda wote ila mwananfunzi anapokuwa tayari ndio anamuona mwalimu kuwa yupo.

Mambo mengi kwenye maisha ambayo hujayawekea mkazo huwezi kuona umuhimu wake, pale unapoyawekea mkazo ndio unaona umuhimu wake na ndio unaona fursa zaidi.

Hivyo kuwa tayari ili uweze kumuona mwalimu wako na unufaike zaidi.

Walimu wapo wengi na kwa uhakika tu walimu wafuatao wanakusibiria wewe uwe tayari ili waanza kukupa yale kuhimu;

AMKA CONSULTANTS

AMKA MTANZANIA

KISIMA CHA MAARIFA

UWEKEZAJI TANZANIA

Hiyo ni baadhi ya mitandao ambayo utajifunz amambo mengi sana kuhusu mafanikio na maisha kwa ujumla.

Chukua hatua sasa, mwalimu anakusubiri.

Thursday, December 4, 2014

Hii Ndio Ardhi Yenye Utajiri Mkubwa Sana Duniani.

Kuna ardhi yenye utajiri na thamani kubwa sana duniani...
Ardhi hiyo sio yenye visima vya mafuta..
Na wala sio ardhi yenye migodi ya madini...
Bali ardhi hiyo ni makaburi,


Makaburi yamejaa ndoto nyingi sana ambazo hazikutimizwa.
Kuna mawazo makubwa ya kibiashara ambayo hayakutimizwa...
Kuna mawazo na ndoto kubwa za mabadiliko ambazo hazikupata nafasi ya kutekelezwa.
Badala yake watu hawa walikufa na ndoto zao.
Angalia na wewe usijekufa na ndoto yako kabla hujaitekeleza,
Maana utainyima dunia kitu kizuri sana.

NENO LA LEO; Maana Halisi Ya Vikwazo.

Obstacles are those frightful things you see when you take your eyes off the goal. –Henry Ford

Vikwazo ni yale mambo ya kutisha unayoyaona pale unapoondoa macho yako kwenye malengo yako makubwa.

Ukishaweka malengo na mipango yako usiangalie tena pembeni, utaona mambo mengi ambayo yatakukatisha tamaa.

Nakutakia siku njema.

Wednesday, December 3, 2014

Lazima Wakufanye Uendelee Kuwa Mjinga...

Ili uendelee kuwaona wao ni muhimu ni lazima waendelee kukufanya wewe mjinga...
Kwa sababu ukijua wanavyojua hutaona umuhimu wao tena...
Huu ndio ukoloni mpya unaoathiri sehemu kubwa ya watu..,
Kudai uhuru wako, unajua cha kufanya.

NENO LA LEO; Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuepuka Kupingwa.

There is only one way to avoid criticism: do nothing, say nothing, and be nothing. –Aristotle

Kuna njia moja pekee ya kuepuka kupingwa; usifanye chochote, usiseme chochote na usiwe chochote.

Vinginevyo chochote utakachofanya lazima kuna mtu atakupinga au kukukosoa.

Fanya kile unachoona ni sahihi kufanya na komaa nacho mapaka ufikie mafanikio.

Nakutakia siku njema.

Tuesday, December 2, 2014

Aina Mbili Za Ujinga.

Kuna aina mbili za ujinga, kulingana na uelewa wa mjinga mwenyewe.
Kuna ujinga wa juu juu ambapo mtu hajui lakini anafikiri kuna mtu anajua.
Na kuna ujinga wa kweli ambapo mtu hajui na anajua hakuna anayejua.
Wanafunzi wana ujinga wa juu juu,
Wataalamu wana ujinga wa kweli.
Hii ndio inatufanya tuwe na kiu ya kutafuta kujua zaidi na hivyo kujifunza zaidi.

Huhitaji Tena Kuomba Ruhusa…

Kuna kipindi ambapo ilikuwa kama unataka kuwa msanii ni lazima uende kwa mzalishaji wa mziki na yeye ndio angeamua kwamba unafaa kuwa msanii au la…

Kuna kipindi ambapo ilikuwa ili uwe mwandishi ungeandika rasimu yako na kuipeleka kwa mhariri na yeye ndio angeamua ichapwe au la…

Nyakati hizo zimepita sasa, huhitaji tena mtu wa kukupa ruhusa kwamba wewe unaweza kuwa msanii au unaweza kuwa mwandishi au hata kitu kingine unachotaka kuwa.

Dunia imebadilika sana kiasi kwamba unaweza kujifunza chochote na kuanza kukifanyia kazi bila ya mtu kukuzuia au kukuruhusu.

Tutumie vizuri mabadiliko haya.

NENO LA LEO; Jinsi Ya Kuua Hofu

If you hear a voice within you say “you cannot paint,” then by all means paint and that voice will be silenced. –Vincent Van Gogh

Kama unasikia sauti ndani yako inayokuambia huwezi kuchora basi kwa njia yoyote ile hakikisha unachora na sauti hiyo itanyamazishwa.

Usikubali kukatishwa tamaa na nafsi yako mwenyewe. Fanya kile unachohofia na hofu itakufa yenyewe.

Natutakia siku njema.

Monday, December 1, 2014

SIKU YA UKIMWI DUNIANI; Mambo Kumi Unayotakiwa Kujua Kuhusu Ukimwi.

Kila tarehe 01/12 ya kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya UKIMWI. Siku hii imepewa heshma yake kutokana na madhara yake makubwa kwa watu wanaoupata.

Wakati tukiwa kwenye siku hii ya UKIMWI jiongeze na mambo haya kumi muhimu.

1. UKIMWI HAUUI.

UKIMWI maana yake ni upungufu wa kinga mwilini. Hivyo kinga yako inapopungua unatoa nafasi ya magonjwa mengine kukushambulia. Hivyo kinachowaua wagonjwa wa ukimwi sio ukimwi wenyewe bali magonjwa nyemelezi.

2. UKIMWI ni tofauti na VIRUSI VYA UKIMWI.

Ukiambukizwa virusi vya ukimwi leo, hauna ukimwi. Unawez akukaa na vizsi hivi kwa muda hata wa miaka kumi na pale kinga ya mwili inaposhindwa kukulinda na magonjwa ndio unakuwa na UKIMWI.

3. Wagonjwa watatu wa kwanza wa UKIMWI Tanzania waligunduliwa katika hospitali ya Ndolange mkoani Kagera mwezi November 1983.

4. UKIMWI husambazwa kwa kupitia maji maji ya mwilini. Yanayoongoza ni damu, na yenye kiasi kidogo ni mate, machozi na majimaji ya ukeni.

UKIMWI TZ

5. Njia kuwa ya kusambaza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine ni kufanya mapenzi bila ya kujikinga. Njia nyingine ni kuchangia vitu vikali kama sindano na pia mama kwenda kwa mtoto.

6. Mpaka leo hakuna tiba wala kinga ya UKIMWI. Baadhi ya tafiti zimeonesha matokeo mazuri ila hakuna ambayo imedhibitishwa kutumiwa kama kinga au dawa.

7. Afrika chini ya jangwa la sahara ndio sehemu yenye maambukizi makubwa ya UKIMWI, asilimia 80 ya watu wenye ukimwi duniani wako Africa chini ya jangwa la sahara. Wakati idadi ya wanachi walioko Afrika chini ya jangwa la sahara ni asilimia 10 tu ya idadi ya watu wote duniani.

8. Wanawake wana hatari mara nane zaidi ya kuambukizwa ukimwi kuliko wanaume.

9. Mikoa inayoongoza kwa UKIMWI Tanzania ni Njombe ukifuatiwa na Iringa na mikoa yenye maambukizi madogo ni Pemba, Unguja na Lindi.

10. Mapambano ya UKIMWI yanaanza na mimi na wewe. Njia nyingine za maambukizi zimeweza kuzuiwa kwa kiasi kikubwa ila njia moja ndiyo yenye changamoto na njia hiyo ni kupitia kufanya mapenzi.

Tushirikiane kuutokomeza UKIMWI.

NENO LA LEO; Kisasi Bora

The best revenge is massive success. –Frank Sinatra

Kisasi bora ni mafanikio makubwa.

Kama mtu amekufanyia jambo baya na unataka kulipa kisasi, kisasi bora kulipa ni kuhakikisha unafanikiwa sana.

Nakutakia siku njema.