Kwa kawaida mtu yeyote anayezaliwa huwa anapitia vipindi tofauti kwenye maisha yake.
Kwanza kabisa anaanza kama mtoto ng’aa, ambapo anakuwa anategemea kunyonya maziwa ya mama tu.
Anaendelea kukua na baadae anakuwa analishwa uji, huku akikazana kutambaa na hatimaye kutembea.
Baada ya muda anaanza kula matonge ya ugali na kukimbia mwenyewe..
Baadae kabisa anakuwa mtu mzima anayejitegemea na kuweza pia kuwasaidia wengine.
Mpaka kufika miaka 53, mtu anatakiwa awe ameshapitia vipindi vingi vya ukuaji na maendeleo kwa ujumla. Na huu ndio umri ambao anakuwa ameshakamilisha mambo mengi kwenye maisha yake na anaishi maisha ya furaha.
Sasa maajabu makubwa ni pale unapomkuta mtu mwenye miaka 53 bado analishwa uji. Yaani yeye tokea atoke kwenye hatua ya kwanza ya kunyonya amekwamba kwenye hatua ya pili ya kunyweshwa uji.
Kama akitishiwa kunyimwa uji huo anaolishwa anaanza kulia sana na kuona maisha yake yatakuwa magumu.
Sio kwamba mtu huyu alizaliwa na ulemavu wa aina yoyote, na wala sio kwamba amekosa nguvu au mbinu nyingine za kujitegemea, yeye amefurahia kulishwa uji na hataki kufikiria zaidi ya hapo.
Ni jambo la kushangaza sana unapomkuta mtu mzima, miaka 53, mwenye afya na nguvu akiendelea kulishwa uji…
0 comments:
Post a Comment