Tarehe 14/12/2014 itakuwa siku muhimu sana katika miaka mitano ijayo. Siku hii itakuwa ni siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Watu wengi sana hawaupi uchaguzi huu nafasi kubwa na wameelekeza macho na masikio yao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hili ni kosa kubwa sana ambalo tunafanya watanzania wenzangu. Uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu kama ilivyo uchaguzi mkuu. Ni kupitia serikali za mitaa ambapo tunakuwa na demokrasia ya moja kwamoja. Yaani kama kuna jambo lolote la kufanya maamuzi kwenye mtaa au kijiji basi wananchi wote watafanya maamuzi kwenye vikao na mikutano mbalimbali.
Pia serikali hizi za mitaa zina mamlaka ya kutunga sheria ndogo ndogo ambazo zinaweza kuwa na athari chanya au hasi kwetu sisi wananchi.
Serikali za vijiji zina mamlaka makubwa sana kwenye ardhi na hivyo zinaweza kufanya maamuzi ya kuuza ardhi kwa watu mbalimbali. Hivyo unapokuwa na serikali ya kijiji ambayo sio imara mnaweza kujikuta mnapoteza ardhi yenu.
Mwisho kabisa naamini mabadiliko na maendeleo ya nchi hii yanaweza kuanzia kwenye ngazi ya mitaa, vitongoji au vijiji. Hii ni kwa sababu matatizo yoyote tunayokumbana nayo kama taifa yanaanzia katika ngazi ya familia na hatimaye mitaa. Kwa mfano wahalifu wote wanaishi kwenye mitaa yetu, wauzaji wa madawa ya kulevya na hata watumiaji wanakaa kwenye mitaa yetu. Hivyo tukiweza kuwa na serikali zamitaa ambazo zipo imara tunaweza kujenga misingi mizuri kama taifa.
Baada ya kuona umuhimu huo mkubwa wa serikali za mitaa sasa naomba nikushirikishe mambo matano muhimu ya kuzingatia kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa.
1. Hakikisha unapiga kura na hamasisha wengine nao wapige kura.
Ule utamaduni wetu watanzania wa kutokupiga kura halafu tunakuwa wa kwanza kulalamika kwamba viongozi ni wabovu sio utaratibu mzuri. Hakikisha unapiga kura siku hiyo ya uchaguzi na pia washawishi ndugu jamaa na marafiki zako nao wapige kura siku hiyo. Kura yako moja ina thamani kubwa sana, usiidharau.
2. Chagua kiongozi mwenye maono na mwenye historia nzuri.
Kwanza kabisa mtu ambaye mtamchagua awe mtu ambaye mnamjua vizuri. Awe ni mtu ambaye amekaa kwenye mtaa huo na mna historia yake nzuri ya namna ambavyo amekuwa akihamasisha mambo mbalimbali kwenye mtaa au kijiji chenu. Awe ni mtu mwenye maono na anayefikiria na kukubali mabadiliko. Kiongozi wa aina hii ataweza kushirikiana nanyi kuleta maendeleo kwenye eneo lenu.
Kujua zaidi kuhusu tabia za viongozi bonyeza maandishi haya.
3. Mtu yeyote atakayotoa rushwa usifikirie mara mbili, usimpigie kura na hamasisha wengine wasimpigie kura.
Uongozi wa serikali za mitaa ni uongozi ambao hauna manufaa makubwa kifedha zaidi ya posho ndogo ndogo. Sasa mtu ambaye anatoa rushwa lili kupata nafasi hiyo, jiulize ananufaikaje? Kwa vyovyote vile atahakikisha akipata nafasi analipa fedha yake aliyowekeza kwa kutoa rushwa hivyo atawaingiza kwenye matatizo.
4. Chagua mtu, usichague chama.
Kwa siasa zetu za Tanzania bado haturuhusu mgombea binafsi hivyo unalazimika kuchagua mgombea anayeletwa na chama fulani. Chama kinaweza kuwa na sera nzuri sana ila kama kitakuwa na mgombea ambaye hana uwezo mzuri wa uongozi sera hizo ni kazi bure. Hivyo hudhuria mikutano ya kampeni, wafatilie vizuri wagombea wote na mchague mtu ambaye unaona anaweza kuleta mabadiliko kwenye mtaa au kijiji chenu. Hata kama wewe ni mkereketwa wa chama fulani ila ukaona mgombea wa chama kingine ana sifa zaidi ya mgombea wa chama chako, mpigie kura. Mwisho wa siku maendeleo yatakuwa ni kwa mtaa wenu na sio chama chenu.
5. Tuoneshe ushirikiano na kuwawajibisha viongozi tuliowachagua.
Baada ya uchaguzi na viongozi kupatikana ni vyema kuweka tofauti za kisiasa pembeni na kupeana ushirikiano ili kiongozi mliyemchagua aweze kutekeleza majukumu yake. Kwa kuonesha ushirikiano mzuri italeta mafanikio makubwa kwa mtaa au kijiji chenu.
Pia pale ambapo kiongozi mliyemchagua anakwenda kinyume na ahadi zake ni vizuri kumwajibisha. Kwenye serikali za mitaa tupo karibu sana na viongozi wetu na hivyo ni rahisi kuhoji mambo mbalimbali ambayo mnaona hayaendi sawa.
Nichukue nafasi hii kuwatakia watanzania wote uchaguzi mwema na twende tukafanye maamuzi sahihi kwa mitaa na vijiji vyetu kwa miaka mitano ijayo.
Tanzania ni yetu sote, tushirikiane kuijenga.
0 comments:
Post a Comment