Jana tarehe 02/11/2014 kulikuwa na mdahalo wa katiba ulioandaliwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere uliokuwa unafanyika katika ukumbi wa ukumbi wa ubungo plaza.
Katika mdahalo huo waliokuwa wajumbe wa iliyokuwa tume ya katiba walialikwa kuzungumza na baadae wananchi waliohudhuria nao wangepata nafasi ya kuzungumzia katiba pendekezwa.
Lengo kubwa la mdahalo huo na mingine ambayo tuliahidiwa itafuata ilikuwa kuwapa uelewa wananchi juu ya katiba pendekezwa kabla wakati wa kupiga kura haujafika.
Binafsi ninaona kitu hiki ni kizuri sana maana taasisi inayoandaa midahalo hii haina uegemeo wowote wa kisiasa na hivyo itatoa nafasi nzuri ya wananchi kujifunza yaliyomo kwenye katiba pendekezwa.
Katika hali ya kushangaza wakati mdahalo unaendelea na Jaji Warioba akizungumza kiliibuka kikundi cha watu ambao walionesha mabango ya kupinga mdahalo ule na kusema kwamba wanaikubali katiba pendekezwa. Hata walipotakiwa kutulia chini ili mdahalo uweze kuendelea bado hawakusikia na hatimaye ikapelekea vurugu kubwa na mdahalo kuahirishwa.
Kwanza kabisa hiki ni kitendo cha ajabu sana ambacho kinatakiw akulaaniwa na kila Mtanzania ambaye ana mapenzi mema na nchi hii. Ni kweli kabisa hatuwezi kukubaliana wote, ila kutofautiana kwetu kifikra na kihoja kusifanye tuonanae kama maadui. Hizi ni siasa chafu na za kitoto sana ambazo naona zinanyamaziwa na wanaofanya ujinga huu wanaonekana kama wanaleta manufaa kwa kikundi fulani.
Kama unaona mtu anakushinda kwa hoja njia sahihi ni kuleta fujo na kupigana? Hapana hii sio njia sahihi kabisa na kama tutaendelea kuacha mambo haya yaendelee tutalipeleka taifa kubaya.
Katiba ni kitu ambacho kinamhusu kila mwananchi na hivyo kila mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni yake na hisia zake juu ya katiba hii. Lakini katika kutoa maoni hayo na hisia hizo usiingilie uhuru wa mwenzako au kuleta fujo au kumwona anayeamini tofauti na wewe ni adui.
Naomba watanzania wote tulaani kitendo hiki kilichotokea na tusitoe tena nafasi ya kutokea kwa kitendo kama hiki.
Tanzania ni nchi yetu sote, tushirikiane kuijenga.
TUPO PAMOJA.
0 comments:
Post a Comment