Ni wakati gani unafikiri unahitaji kuanza kuonesha tabia za uongozi? Unapoambiwa umepewa nafasi ya kuwa meneja? Au unapoteuliwa kuwa mwakilishi wa watu au msimamizi wa sekta fulani? Yote hayo yanaweza kukupa nguvu ya uongozi ila hayawezi kukufanya kiongozi kama hukuwa kiongozi kabla. Na vibaya zaidi ni kwamba nguvu hii ya uongozi huisha mara moja pale nafasi hiyo inapoondoka.
Huhitaji cheo ili kuwa kiongozi, unahitaji kutumia uwezo wako na vipaji vyako katika maisha yako ili kuwa kiongozi. Unahitaji kutimiza wajibu wako na kufanya zaidi ya unavyotegemewa kwenye kazi, biashara na hata kwenye maisha yako. Kwa kufanya hivi ndio utajitengeneza kama kiongozi ambapo wengine watafurahia kukufuata.
Ili kuwa kiongozi huhitaji cheo, unahitaji kufanya maamuzi ya kuwa kiongozi kisha kuanza kuongoza. Kila mtu anayo nafasi ya kuwa kiongozi ila wachache ndio wanaochagua kuwa viongozi. Kama kila mtu angefagia mtaa wake dunia nzima ingekuwa safi sana. Ila kwa kuwa wengi hawafanyi wanayopaswa kufanya tunaishia kuwa na matatizo mengi duniani.
Nguvu nne za uongozi ambazo hazihitaji cheo.
Kama unajiuliza unawezaje kuwa kiongozi bila ya kuwa na cheo soma nguvu hizi nne za uongozi ambazo tayari unazo bila hata ya kuwa na cheo. Kwa kufanya mambo haya manne ambayo hayahitaji cheo kutakutengeneza kuwa kiongozi mzuri kwenye maisha yako.
1. Una uwezo wa kwenda kwenye shughuli zako, iwe kazi au biashara na kufanya kazi kwa moyo mmoja na ubunifu wa kipekee kitu ambacho kitakufanya utoe majibu mazuri sana. Una uwezo wa kuamua kuwa bora siku ya leo zaidi ya ulivyokuwa bora siku ya jana na huhitaji kuwa na cheo ili kufanya hivyo. Kwa kutimiza wajibu wako na kuongeza ubora kila siku unakuwa kiongozi ambaye wengine watapenda kukufuata.
2. Leo hii unao uwezo wa kushawishi na kuchochea watu wanaokuzunguka ili wafanye mambo ambayo yatawasaidia kuboresha kazi zao na maisha yao kwa ujumla. Huhitaji kuwa na cheo ndio uweze kumshawishi mtu kwamba akifanya juhudi kwenye kazi zake ataboresha maisha yake. Unahitaji kumuonesha picha kubwa na kumchochea aweze kuifikia, kama na wewe unaelekea kuifikia au umeshaifikia.
3. Unao uwezo wa kuleta mageuzi chanya kwenye mazingira hasi. Hata mazingira ya kazi au maisha yawe magumu kiasi gani unao uwezo wa kubadili mtazamo wako na wa wanaokuzunguka kuhusu mazingira hayo. Huhitaji cheo kuweza kuangalia faida unayoweza kupata kwenye mazingira fulani zaidi ya kuangalia hasara tu. Pia huhitaji cheo kubadili mazingira mambovu ambayo yanakukandamiza wewe au wale wanaokuzunguka.
4. Una uwezo wa kuwa mwema kwa wale wanaokuzunguka kwenye shughuli zako na maisha yako kwa ujumla. Huhitaji cheo ndio uweze kuwaheshimu, kuwajali na kuwapenda watu wanaokuzunguka kwenye maisha yako. Kwa kufanya hivyo utawafanya watu hawa kufurahia kuwa karibu na wewe na kuona maisha yao yana thamani kubwa. Mtu anayeona thamani kubwa ya maisha yake anaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yake na shughuli zake.
Mambo haya manne hayahitaji cheo ndio uweze kuyafanya. Hebu anza kuyafanya mara moja kwenye maisha yako na utaona mabadiliko makubwa. Kumbuka wewe ni kiongozi hata kama huna cheo.