Jiunge Hapa Kupata Makala Mpya Inapotoka!

We'll not spam mate! We promise.

Sunday, February 23, 2014

Lengo Langu Kubwa Kwenye Maisha; Kuwa Rais wa Tanzania.

  Leo nakushirikisha lengo kubwa sana kwenye maisha yangu. Lengo hilo ni kuwa rais wa nchi yangu Tanzania. Kama ilivyo kwenye kuweka lengo lolote kuna hatua muhimu za kufuata ili kuweza kufikia lengo unaloweka.   Katika lengo langu mimi ninachotaka ni kuwa rais wa nchi yangu Tanzania.

  Kwa nini nataka kuwa rais wa tanzania?

Kuna sababu nyingi zinazonisukuma kutaka kuwa rais wa nchi yangu. Hapa nitaeleza sababu chache na kadiri muda unavyokwenda nitazidi kueleza sababu nyingine.

1. Naipenda nchi yangu na ninatamani kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha ya wananchi na taifa kwa ujumla. Naamini nina mchango mkubwa sana kwenye mabadiliko ya nchi yangu na njia nzuri ya kutoa na kutekeleza mchango huo ni kupata nafasi kubwa kwenye uongozi wa nchi hii.

2. Naamini matatizo mengi tuliyonayo Tanzania yanaweza kutatulika kama tukiwa na viongozi ambao wana uzalendo.

3. Naamini viongozi wengi tulionao sasa hivi hawana sifa za uongozi na wengi wapo kwa maslahi binafsi hivyo wanazidi kuwa tatizo kwenye nchi yetu.

4. Naamini maendeleo ya nchi yanatokana na maendeleo ya wananchi ambao wamejengewa uwezo na sio kutokana na misaada ama mikopo.

5. Naamini mifumo mingi ni mibovu na hatuwezi kubadili nchi hii bila kubadili kabisa mifumo hiyo. Kwanza ni mfumo mzima wa uongozi, pili mfumo wa utumishi wa umma, tatu mfumo wa elimu. Mifumo hii hasa wa elimu na uongozi imekuwa kikwazo kikubwa kwetu kupata taifa ambalo linajielewa.

 

Ni lini nategemea kuwa rais wa nchi hii?

Nategemea kuwa rais wa nchi hii ifikapo mwaka 2040. Ni mbali sana lakini nina sababu za msingi za kuweka muda huo mwingi mpaka niwe raisi. Kuanzia leo mwaka 2014 mpaka kufika mwaka 2040 ni miaka 26 kuna mambo mengi sana nahitaji kuyafanya katika miaka hiyo ndio niwe rais wa Tanzania.

 

Kwa nini nimetangaza mapema na kwa nini nakuambia wewe?

1.Nimetangaza mapema na nimeweka wazi ili kupata muda wa kutosha kujiandaa. Najua kazi ya urais sio kazi lele mama, ni kazi inayohitaji busara kubwa na uwezo mkubwa wa kuamua na kutenda. Hivyo kwa miaka 26 ijayo nitajifunza mambo mengi sana ya uongozi ili niwe kiongozi bora na ninayejua ni kitu gani ninafanya.

2. Nataka nijue ni watu gani ninaoweza kufanya nao kazi. Kama rais wa nchi nitahitaji wasaidizi ambao nitawachagua mimi. Nitakapokuwa rais nitatumia vigezo vikali sana kuchagua watu watakaoshika sehemu za uongozi. Sitotumia kujuana au urafiki, nitatumia uwezo wa mtu. Naamini kwenye miaka hii 26 nitakutana na watu wengi na nitaweza kupima uwezo wao hasa kwenye matendo. Kama wewe ni rafiki yangu na unasoma hapa ni vyema ukawa unaonesha uwezo wako kwenye mambo yako binafsi unayofanya. Hata kama tumewahi kulala kitanda kimoja usishangae ukija kukosa nafasi hata ndogo sana wakati nitapokuwa rais.

3. Nahitaji mchango wako ili niweze kuwa kiongozi bora. Nahitaji ushauri wako, na nahitaji kupingwa ninapotoa hoja ambazo haziendani na mahitaji yetu. Naamini haya yote yatanijenga kuwa kiongozi bora.

 

Kwa sasa nitatumia blog hii kama sehemu ya kujifunza uongozi. Nakukaribisha twende pamoja kama na wewe una ndoto ya kuwa kiongozi kwenye maisha yako. Kila siku ya jumapili nitakuwa naweka makala moja inayohusisha UONGOZI, SIASA AU RAIS KIVULI. Pia nitakuwa nashirikisha watu vitabu mbalimbali vya uongozi nitakavyokuwa navisoma.

Karibu tujiandae kulijenga taifa letu.

Nategemea maoni yako hapo chini.